Derby ya mashemeji kitaumana usiku

Muktasari:

  • Mara ya mwisho mechi ya Ligi Kuu Kenya kupigwa usiku ilikuwa ni Oktoba 23,2011 kwenye uwanja huo huo wa Nyayo ambao ilizikutanisha timu hizo na Gor Mahia kushinda 1-0 huku ikishuhudiwa vurugu kubwa ambazo zilisababisha vifo vya mashabiki saba.

Wakati homa ya mchezo wa dabi ya Mashemeji kati ya Gor Mahia FC na AFC Leopards ikizidi kupamba moto, Shirikisho la Soka nchini Kenya (FKF) tayari limeweka wazi kuwa mchezo huo utapigwa usiku.

Mchezo huo wa Ligi Kuu Kenya ambao unasubiriwa kwa hamu na wapenzi wa soka Afrika Mashariki utapigwa Jumapili hii ya Aprili 21 kwenye Uwanja wa Nyayo uliopo jijini Nairobi kuanzia saa 3:00 usiku.

Mara ya mwisho mechi ya Ligi Kuu Kenya kupigwa usiku ilikuwa ni Oktoba 23, 2011 kwenye uwanja huo huo wa Nyayo ambapo Gor au K'Ogalo ilishinda kwa bao 1-0 huku ikishuhudiwa vurugu kubwa ambazo zilisababisha vifo vya mashabiki saba.

Mbali na vifo hivyo vya kusikitisha, wengine 20 waliachwa wakiwa wamejeruhiwa vibaya katika usiku huo wa maafa ambao uliacha alama isiyofutika kwa soka la Kenya.

Katika mchezo wa Jumapili, Gor Mahia FC inapewa nafasi kubwa ya kushinda dhidi ya Leopards ambao ni maarufu pia kama Ingwe, na kuendelea kujitengenezea mazingira mazuri ya kutetea ubingwa huku ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Leopards katika mchezo wa mzunguko wa kwanza ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Kasarani.

Mwenendo mzuri wa kocha Jonathan Mckinstry ndani FKFPL, unaibeba K'Ogalo kwani katika mechi 26 alizoingoza imekusanya alama 54 baada ya kushinda mechi 15, sare tisa na kupoteza mbili huku ikifunga magoli 33 na kufungwa 12 tofauti ya alama 16 dhidi Leopards inayoshika nafasi ya nane kwa alama 38.

Wengi wanasubiri kumuona nyota Benson Omalla wa Gor Mahia mwenye mabao 12 kama ataendelea kujitengenezea njia ya kuwania kiatu cha ufungaji bora baada ya kukosa msimu uliopita akifunga 26 na kuzidiwa bao moja na Elvis Rupia kutoka Kenya Police FC ambaye kwa sasa anakipiga Ihefu FC inayoshiriki Ligi Kuu Bara kwa kufunga mabao 27.

Hamasa na tambo mbalimbali zimezidi kuwa kubwa kutoka kwa viongozi na wapenzi wa timu zote ambapo leo, Aprili 18 imeshuhudiwa shabiki wa Gor Mahia FC, Eliud Owalo ambaye pia ni waziri wa Mawasiliano nchini Kenya ametembelea mazoezi ya timu hiyo na kutoa motisha ya fedha kwa wachezaji.

Festus Chuma ni mwandishi wa habari za michezo kutoka Kenya ameiambia Mwanaspoti kwamba ukiachana na presha iliyopo nje ya uwanja kuanzia kwa viongozi, mashabiki, mitandao ya kijamii na vituo mbalimbali vya habari nchini humo, anadhani itakuwa moja kati ya mechi bora ambapo kwake anaamini dakika 90 zitakamilika kwa sare.

Viingilio vya mchezo huo vimetajwa kuwa ni Ksh1000 kwa VIP, mzunguko ikiwa ni 300 ambapo vituo vya kuuza tiketi vitakuwa Kenya Cinema (CBD), Nairobi City Stadium, Riadha House na nje ya uwanja wa Nyayo.

Katika mechi tatu za mwisho za Ligi Gor Mahia FC imeshinda moja sawa na mechi ambayo imepoteza sawa pia na sare iliyotoka mechi hizo ni dhidi ya Bandari (1-0), Kakamega Home Boys (0-0) na Nzoia Sugar (1-3).

Leopards nayo imeshinda mbili na kutoka sare moja dhidi ya Shabana (0-1), Sofapaka (1-1) na Posta Rangers (0-1), ambapo pia katika mechi zote 26 za Ligi timu hizo zilizocheza hadi sasa kipa wa Gor Mahia FC, Kevin Omondi ajaruhusu bao katika mechi 17 huku Levis Opiyo wa Leopards yeye hajaruhusu kwenye mechi tisa.