Shirko, kutoka muziki hadi ndani ya Serikali ya Rais Ruto

MOMBASA. Unapoizungumzia Yamoto band hukosi kumtaja kijana mtayarishaji wa mziki ‘producer’ Awadh Salim Awadh maarufu Shirko. Huyu ni mzaliwa Mombasa nchini Kenya ambaye alibahatika pia kuishi nchini Tanzania.

Mbali na kuwa muandaaji wa mziki mwaka 2000 alitambulika rasmi kwenye mziki wa kizazi kipya na ngoma ya ‘Na wewe tu’ ya kwao 2Berry waliomshirikisha huku mawazo na muundo wa ngoma hiyo iweje akitoa yeye ambapo verse yake alitumia lugha ya kiingereza.

Akipiga story na Mwanaspoti anasema kipaji chake kiligundulika akiwa anasoma ambapo walikuwa wanaongoza makundi ya burudani za kidini ‘Madrasa’ ambapo alikuwa mpiga filimbi za chuoni zenye asili ya waarabu. Akiwa kama mtayarishaji wa mziki aliweza kufanya kazi na zaidi ya wasanii 30 kutoka Tanzania na wengi wao wakiwa na majina makubwa ukiachana na Yamoto Band na wasanii wengineo kutoka Kenya

Anasema baada ya kumaliza masomo hakuwa na kazi ya kufanya licha ya kupenda mziki wa kizazi kipya na hivyo alishawishiwa na rafiki zake waliokuwa wakiunda kundi la ‘Lovely brother LB’s’ kujiunga nao ambapo walitumia baadhi ya mashairi aliyokuwa akiandika kushiriki mashindano ya kuimba na kufika nusu fainali na kuwafanya wamlazimishe kuwa mmoja wa kundi hilo rasmi.


Mwandishi:Na wewe tu ndio nyimbo iliyokutambulisha rasmi kwenye mziki ilikuwaje hadi kufanya ngoma ile?


Shirko: Nyimbo ina historia kubwa, nakumbuka Berry White aligoma kuweka verse kwa sababu ilikuwa studio ndogo na haina jina, pia aliona underground sana. Baadaye baada ya kuisikiliza alidhani ni Redsan na alishangilia ila baada ya kujua ukweli alipooza na kwa bahati nzuri producer Alan Mapigo alilazimisha niingize back vocal za kwenye verse ya ngoma ile na pia wakapendekeza verse yangu ibakie vile vile tofauti na alivyotaka Berry White na kupelekea ile ngoma kuwa kimataifa.Mwandishi: Ilikuwaje hadi kuishi Tanzania?


Shirko: Wazo lilikuja baada ya Berry Black kumshauri kaka yake kuwa kuna producer Mombasa anajua kazi na angependa nihamie Zanzibar kufanya na wao kazi na ndipo nilipomuomba baba yangu ruhusa na alikubali kisha tukaanza kutafuta vibali kwa kushirikiana na dada yangu ambaye niliishi naye na kwa sasa hayupo tena duniani.


Mwandishi: Nini kilikuvutia kufanya collabo na wasanii wa Tanzania?


Shirko: Wasanii wa Tanzania wanajua hili halina kipingamizi, pili wanaheshimu kipaji cha mtu, kama unajua haogopi kukuambia unajua anakupa sifa zako bila kufikiria mara mbili au kusita kufanya kazi na wewe.


Mwandishi: Kwani kwa Kenya hali ikoje?


Shirko: Nimeishi Tanzania nimeona wengi wapo hivyo labda wachache tu ndio wapo tofauti ila wengi wapo tu real. Kwetu (Kenya) bado kuna choyo ya maendeleo, wivu na uoga wa kuhofia kupitwa na yule ambaye unaogopa asije kukupiku muda wowote, japo kiuhalisia kila mtu ana bahati, daraja, nafasi na utofauti wake kwenye kipaji chake.


Mwandishi: Ilikuwaje hadi kufanya kazi na Yamoto Band?


Shirko:  Nilitaka kujiunga pale TipTop, nilimfuata meneja Babutale kutaka anisimamie kwa nafasi yoyote ile ambayo ningeweza kuipata ila sikufanikiwa kutokana na mtazamo wake. Kwanza alitaka wasanii wanaoanza ambao hawajafika hatua yoyote kwenye sanaa yao, kwangu aliona labda tayari nishakuwa maarufu kwa kiasi fulani akaniambia hawezi kunipokea. Baada ya hapo nilienda kwa Mkubwa Fella alinipokea na kuniambia tufanye kazi.


Mwandishi: Ilikuwa mwaka gani?


Shirko: Ilikuwa 2012 baada ya kuja nyumbani Mombasa nikarudi Dar es Salaam tukafungua studio kwa mara nyingine baada ya wao kuacha kufanya kazi na producer Sulesh aliye kuwa producer wa Mkubwa na Wanawe hapo awali.

Nilikuta wasanii wasiopungua 120 na wote walitamani kutoka kimziki wakiamini mimi ndio daraja lao la matumaini.

 Kabla tulifanya kazi nyingi sana baadaye nikaanzisha ubunifu wa kutengeza makundi sababu niliona kufanya kazi na msanii mmoja mmoja ingenielemea ndipo nikaja na wazo la kuwachagua wasanii baada ya kuunda beat ya dance bongo fleva iliyozaa nyimbo “Yamoto” niseme tu mimi ndio niliyebuni kundi na muanzilishi.


Mwandishi: Mafanikio gani uliyapata baada ya kufanya kazi na Yamoto band?


Shirko: Iliniletea watu tofauti wenye majina makubwa na wengi walipenda ile staili ya muziki niliobuni na kuufanya rasmi kuwa mziki wa Yamoto band.

Hata hivyo nilipata connection nyingi kupitia kampuni kadhaa Tanzania, Kenya na Afrika kusini kwa kuandaa matangazo kwa njia ya utayarishaji muziki na pia wasanii wa kutoka Ivory Coast walinitafuta kutaka kufanya kazi na mimi. Pia nimewahi kuhusishwa kwenye tuzo mbalimbali za kimataifa bila matarajio. Nimeweza kusafiri nchi mbali mbali na kupata mapokezi makubwa na kukaa na wafanyibiashara wakubwa kitu ambacho sikuwahi kutarajia kama ningefikia hatua hiyo.


Mwandishi: Nini kilipelekea Yamoto Band kuvunjika?


Shirko: Kulisababishwa na maslahi tu, kila mmoja alifikia hatua na kuona anaweza kufika mbali akiwa peke yake, Ilifikia hatua pia maboss walikuwa wanaenda slow kuwabrand wasanii kileo zaidi walitumia mifumo ya kizamani ambayo miaka ilishabadilika na mashabiki walikua wanataka kuona wasanii wao wapo katika level za wasanii fulani ambao wapo level moja kiushindani.

Hii ilipelekea hadi Rayvanny aliyekuwa anawatazama Yamoto band kama kioo kwake kuanza kufika kimataifa wa kwanza na kuwa mkubwa kuliko Yamoto band na kufanya vijana waone wanacheleweshwa kwani walitaka wafike level zile kabla ya Rayvanny. Namtolea mfano Rayvanny kwa sababu ni mmoja wa wasanii waliokuwa wamejibrand kuliko Yamoto Band licha ya kuwa wao walikuwa wapo juu kibiashara ya muziki na wenye mashabiki wengi kuliko wasanii wengi Afrika Mashariki.


Mwandishi: Kuvunjika kwa Yamoto Band kulikuathiri kama muasisi na mtayarishaji wa mziki?


Shirko: Iliniathiri kikubwa sana maana baada ya kuyumba na kujitahidi sana kutafuta tobo la maisha kwenye safari yangu ya utayarishaji muziki niliamini kuwa kwa kupitia mafanikio yao ningebadili maisha yangu kwa kiasi lakini ilikuwa tofauti kwani sio ulipangalo wewe litakuwa katika mipango anayoitaka Mungu.

Nilivyoona tu mapema utengano unaanza nilijipanga kabisa japo niliondoka kwa kuchelewa ila kwa sababu zangu binafsi na sio kwa sababu ya kuvunjika kundi la Yamoto band.


Mwandishi: Ni ngoma gani uliyoizalisha hadi wewe mwenyewe ukiisikia unafeel kweli ulituliza akili?


Shirko: Ngoma niliyoitengeneza mpaka nikasema hapa kweli nimetengeneza nyimbo na nusu ni tofauti na nyimbo ambayo ilinila mafanikio hizi ni nyimbo mbili tofauti. Niliyoitengeza na hadi mwenyewe nikaivulia kofia ni ‘Nibebe’ ya kwake Aslay na iliyonipa mafanikio zaidi ni ‘Na wewe tu’ (nataka kuwa nawe) ya kwao 2 Berry waliyonishirikisha.


Mwandishi: Unajisikiaje kama kijana aliyeaminiwana Rais William Ruto hadi kupewa nafasi ndani ya serikali katika upande wa sanaa?


Shirko: Ni jambo kubwa sana kumshukuru Mungu kujikuta nimekuwa na bahati ya kuaminiwa na Rais William S. Ruto hadi kupata kitengo cha kupambania sanaa kupitia Wizara ya Sanaa, Mambo ya Vijana na Michezo na kuorodheshwa kwenye kamati ya wabunifu na kutoa mawazo ya kuleta mabadiliko katika tasnia nzima. Hili sio jambo la kawaida kwa mtu wa kawaida kama mimi. Nimshukuru Mungu na nchi yangu pamoja na Waziri Abab Namwamba waliona nilikuwa na kitu fulani na wakaona mchango wangu ngeongeza kitu gani kwenye sanaa na kuleta mabadiliko.