Sare yaipa matumaini Harambee Stars
Muktasari:
- Mechi hiyo iliyokuwa ya kuvutia kwa pande zote mbili, iligeuka na kuwa mtihani mgumu kwa Kenya baada ya kiungo Marvin Nabwire kutolewa nje kwa kadi nyekundu katika dakika ya 21, jambo lililowalazimu kucheza wakiwa pungufu kwa zaidi ya dakika 70.
HARAMBEE Stars ya Kenya, imeonyesha kuitaka robo fainali ya michuano ya CHAN 2024 baada ya kulazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Angola kwenye mechi ya Kundi A iliyopigwa Alhamisi usiku katika Uwanja wa Kimataifa wa Moi, Nairobi huku kocha wa timu hiyo akiwasifu wachezaji.
Mechi hiyo iliyokuwa ya kuvutia kwa pande zote mbili, iligeuka na kuwa mtihani mgumu kwa Kenya baada ya kiungo Marvin Nabwire kutolewa nje kwa kadi nyekundu katika dakika ya 21, jambo lililowalazimu kucheza wakiwa pungufu kwa zaidi ya dakika 70.
Licha ya changamoto hiyo, vijana wa kocha Benni McCarthy walikuwa imara na kuibuka na pointi muhimu iliyowaweka kileleni mwa kundi.
Angola ilianza kwa kasi na kufunga bao la kuongoza la dakika ya 7 tu kupitia Jó Paciência, bao lililowapa nguvu wageni huku likiwanyamazisha mashabiki wa nyumbani kwa muda.
Kenya haikukata tamaa, na dakika tano baadaye ilipata nafasi ya kusawazisha baada ya VAR kuthibitisha madhambi yaliyofanywa na beki Mafuta ndani ya eneo la hatari.
Austin Odhiambo alipiga mkwaju huo wa na penalti na kuisawazishia Kenya, likiwa bao lake la pilikwenye mashindano hayo.
Kocha McCarthy alisifu nidhamu na moyo wa kupambana wa wachezaji wake, akisema sare hiyo ni ishara ya ukuaji wa kiushindani ndani ya kikosi hicho. Kwa upande wa Angola, mechi dhidi ya Zambia itakuwa ya ‘kufa au kupona’ katika harakati zao za kufuzu.
Kenya sasa inajiandaa kuivaa Morocco katika mechi inayofuata, ambapo hata sare inaweza kuwaweka kwenye mazingira mazuri ya kufuzu kwa hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza.
Kwa matokeo hayo, Kenya imepanda kileleni mwa Kundi A ikiwa na pointi nne baada ya mechi mbili, ikiwazidi Morocco na DR Congo zenye pointi tatu kila mmoja. Angola inasalia na pointi moja na inakabiliwa na kibarua kigumu cha kushinda mechi ijayo dhidi ya DR Congo ili kusalia katika fainali hizo za nane zilizoandaliwa kwa pamoja na nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.