Pamba jiji yavuta golikipa Mkenya
Muktasari:
- Ochieng aliyesaini mkataba wa miaka miwili ndani ya Pamba Jiji, anaungana na Wakenya wenzake ambao wapo benchi la ufundi la timu hiyo likiongozwa na kocha mkuu, Francis Baraza pamoja na kocha wa makipa, John Waw ambaye pia yupo ndani ya benchi la ufundi la timu ya taifa ya wanawake ya Kenya chini ya umri wa miaka 17.
IMEELEZWA kwamba, Pamba Jiji tayari imekamilisha usajili wa kipa Steve Ochieng kutoka Shabana FC ya Kenya kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo msimu ujao wa 2026-2027.
Ochieng aliyesaini mkataba wa miaka miwili ndani ya Pamba Jiji, anaungana na Wakenya wenzake ambao wapo benchi la ufundi la timu hiyo likiongozwa na kocha mkuu, Francis Baraza pamoja na kocha wa makipa, John Waw ambaye pia yupo ndani ya benchi la ufundi la timu ya taifa ya wanawake ya Kenya chini ya umri wa miaka 17.
Mwanaspoti limepata taarifa za ndani kutoka kwa kigogo mmoja wa Pamba Jiji, aliyesema ujio wa Ochieng ndani ya kikosi hicho, unakwenda kuziba pengo la Yona Amos.
Amos aliyemaliza msimu wa 2025-2026 akiwa na cleansheets nane ndani ya Ligi Kuu ya NBC baada ya ule wa 2024-2025 kuwa nazo 11, inaelezwa kwamba tayari alishasaini mkataba na Singida Black Stars.
Kigogo huyo amesema: “Tumeamua kumsajili Ochieng kwani ni kipa mzuri na msimu uliyoisha katika Ligi Kuu ya Kenya alimaliza na cleansheets 15, tunaamini ni mbadala sahihi wa Yona Amos.”
Mbali na Ochieng, kuna taarifa zingine kuhusiana na timu hiyo kusaka kiungo wa kigeni mbadala wa Kelvin Nashon aliyejiunga na klabu ya Simba.
“Wachezaji wengi wanaondoka, wapo waliomaliza mikataba na wale ambao tutaona wakapate changamoto mpya timu nyingine, hivyo tutasajili wachezaji wengi,” amesema.