Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu Harambee Stars kutimkia Uturuki kucheza mechi mbili za kirafiki

Muktasari:

  • Hii itakuwa ni mara ya pili Harambee Stars kucheza mechi nchini Uturuki, awali ilikuwa Oktoba 16, 2023, walipotoka sare ya 2-2 dhidi ya Urusi, mechi ambayo ilikuwa ya pili kwa Kenya kuikabili timu ya Ulaya baada ya kutoka 0-0 na Uswisi jijini Nairobi, Desemba 6, 1983.

TIMU ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars inakwenda nchini Uturuki kucheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa zilizo katika Kalenda ya FIFA dhidi ya Senegal na Equatorial Guinea huku sababu za kufanya hivyo zikitajwa.

Hii itakuwa ni mara ya pili Harambee Stars kucheza mechi nchini Uturuki, awali ilikuwa Oktoba 16, 2023, walipotoka sare ya 2-2 dhidi ya Urusi, mechi ambayo ilikuwa ya pili kwa Kenya kuikabili timu ya Ulaya baada ya kutoka 0-0 na Uswisi jijini Nairobi, Desemba 6, 1983.

Mechi hizo zimepangwa kuchezwa Antalya, mji ambao Kenya pia ilicheza dhidi ya Urusi miaka miwili iliyopita. Harambee Stars itaanza dhidi ya Equatorial Guinea (Novemba 14, 2025), kisha Senegal (Novemba 18, 2025).

Kwa mujibu wa Athanas Oballa, Mkuu wa Miradi na Timu za Taifa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF), mechi hizo zimepangwa kufanyika Uturuki kwa sababu eneo hilo lina urahisi wa kufikika kwa wachezaji wa Equatorial Guinea na Senegal wanaocheza soka barani Ulaya.

“Kucheza mechi hizo Uturuki kutarahisisha usafiri na maandalizi kwa Equatorial Guinea na Senegal kuliko kama tungecheza Afrika. Itakuwa rahisi kwao kupata safari za kuunganisha ndege,” amesema Oballa na kuongeza.

“Inawezekana mechi zikachezwa bila mashabiki.”

Baada ya kuivaa Kenya, Equatorial Guinea itacheza mechi ya pili dhidi ya Madagascar, Novemba 17, 2025 hukohuko Antalya.

Kwa upande wa Senegal, watatua Uturuki wakitokea Uingereza, baada ya kucheza na mabingwa wa dunia mara tano, Brazil kwenye Uwanja wa Emirates jijini London, Novemba 15, 2025.

Harambee Stars na Senegal hazijawahi kukutana katika mechi ya kirafiki, lakini zimewahi kukutana mara nne katika michuano ya AFCON, ambapo Senegal ilishinda 3-0 mwaka 2019, 2004, na 1992, huku mechi ya AFCON 1990 ikimalizika kwa matokeo ya 0-0.

Mechi hii ya kirafiki inakuja baada ya ziara ya Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, nchini Kenya, Oktoba 20, 2025, akiwa miongoni mwa wageni waalikwa katika maadhimisho ya Siku ya Mashujaa yaliyofanyika Kitui.

Oktoba 21, 2025, Rais wa Kenya, William Ruto, alitangaza kuwa yeye na mwenzake wa Senegal wamesaini makubaliano ya kuondoa masharti ya viza baina ya nchi hizo mbili, huku akifichua nchi hizo kuanza kushirikiana katika sekta ya michezo, ambapo Kenya itafaidika na utaalamu wa Senegal katika uendelezaji wa miundombinu, usimamizi wa matukio, na ujenzi wa urithi wa michezo kuelekea maandalizi ya AFCON 2027, ambayo Kenya itashirikiana kuandaa na Tanzania na Uganda.

“Kwa kuchanganya nguvu za Kenya katika riadha na ubabe wa Senegal kwenye soka, tunalenga kuinua vijana wetu na kuimarisha diplomasia ya kitamaduni,” amesema Ruto.

Hata hivyo, Oballa alisisitiza kwamba mechi dhidi ya Senegal haina uhusiano wa moja kwa moja wa kisiasa au kidiplomasia, bali ni mpango wa kibiashara wa soka.

“Mechi hii ni biashara ya soka na sidhani kama serikali ya Kenya au Senegal zimehusika,” amesema Oballa.

“Mechi zetu za kirafiki dhidi ya Equatorial Guinea na Senegal zimepangwa na McSport, shirika maarufu la kupanga mechi lililoidhinishwa na FIFA.”

“McSport imekuwa ikipanga mechi za kirafiki kwa timu nyingi kubwa za Afrika na wao ndio waliopanga pia mechi zetu mbili dhidi ya Chad mwezi Juni,” ameongeza.

Kama kielelezo cha kibiashara katika upangaji wa mechi hizo, katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Harambee Stars imecheza mechi moja tu ya kirafiki nchini Kenya dhidi ya Sudan Kusini, Septemba 2023. Mechi nyingine tisa wamezicheza nje ya Kenya katika nchi za Iran, Malawi, Mauritius, Morocco, Qatar, na Uturuki. Vivyo hivyo, Senegal imecheza mechi mbili tu za kirafiki nyumbani katika kipindi hicho.

Kwa upande wa kiufundi, Oballa amesema anatarajia Harambee Stars kuonyesha kiwango bora dhidi ya Equatorial Guinea, ambao Kenya waliwafunga 1-0 katika mchezo wao wa mwisho mwaka 2018, na pia dhidi ya Senegal.

“Itasaidia kuongeza hadhi yetu na nafasi yetu katika viwango vya Fifa,” amesema, kabla ya kuthibitisha kwamba Harambee Stars watasafiri kuelekea Uturuki asubuhi ya Jumatano Novemba 12, 2025.