Rais Ruto aipa AFC Leopards Sh2 bilioni
Muktasari:
- Ruto aliweka wazi uamuzi huo alipowakaribisha wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa klabu hiyo katika Ikulu ya Nairobi kwa mazungumzo maalumu yaliyolenga mustakabali wa timu hiyo.
NAIROBI, KENYA: RAIS wa Kenya, William Ruto, ameipa klabu ya AFC Leopards sababu ya kutabasamu baada ya kutangaza kuongeza udhamini wa kila mwaka wa timu hiyo hadi kufikia Ksh100 milioni (takribani TSh2 bilioni), ikiwa ni maandalizi ya msimu wa 2026/27.
Ruto aliweka wazi uamuzi huo alipowakaribisha wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa klabu hiyo katika Ikulu ya Nairobi kwa mazungumzo maalumu yaliyolenga mustakabali wa timu hiyo.
Awali, AFC Leopards ilikuwa ikipokea Ksh75 milioni kwa mwaka, lakini sasa kiasi hicho kimeongezwa kwa Ksh25 milioni, hatua iliyopokewa kwa furaha kubwa na mashabiki wa klabu hiyo maarufu kwa jina la ‘Ingwe’.
Mbali na kuongeza udhamini, Rais Ruto alitangaza zawadi ya Ksh10 milioni taslimu (Tsh203.8 milioni), ambapo Ksh5 milioni zitatolewa moja kwa moja kwa wachezaji kama motisha, huku Ksh5 milioni zilizobaki zikielekezwa kwenye usajili wa nyota wapya kwa ajili ya kuimarisha kikosi.
Aidha, serikali ya Kenya imeahidi kushirikiana na klabu hiyo kuboresha viwanja vya mazoezi pamoja na miundombinu mingine muhimu ili kuiwezesha AFC Leopards kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya ndani na kimataifa.
Hatua ya Rais Ruto kuendelea kuzisaidia kifedha klabu kubwa kama AFC Leopards na Gor Mahia imekuwa ikielezwa kuchangiwa na ukubwa wa mashabiki wa timu hizo, mchango wake katika maendeleo ya soka la Kenya, pamoja na sera za serikali za kuziunga mkono taasisi zenye ushawishi mkubwa katika jamii.