Prime
AFCON 2027 itakuta wachezaji wetu wakiwa taabani
RAIS wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Wallace Karia amezitahadharisha klabu za Ligi Kuu Bara kusajili wachezaji wengi ili kukabiliana na ugumu wa ratiba msimu ujao.
“Tunawaomba kabisa; walimu, viongozi, wasemaji wa timu, waache zile habari za wachezaji wanachoka. Na ndiyo maana tumetoa ruhusa ya kusajili wachezaji 40.”
Karia aliyasema hayo wakati wa hafla ha uzinduzi wa mfumo wa kidigitali wa kusimamia ligi na ugumu unaozungumzwa hapa ni mfululizo wa mechi za karibu karibu na safari ndefu katikati yake kutoka kituo kimoja hadi kingine.
Hii inatokana na uwepo wa fainali za AFCON nchini mwaka 2027, hivyo msimu wa soka lazima uishe mapema ili kutoa nafasi kwa mashindano hayo makubwa zaidi Afrika.
Hapa ndipo kwenye hofu ya PUMZI yetu ya leo.
Tanzania siyo Rwanda au Burundi, nchi ndogo kwa eneo. Nchi yetu ni kubwa ikiwa na eneo la kilomita za mraba takribani 947,300.
Tanzania ni kubwa takribani mara 36 kwa Rwanda, takribani mara 34 kwa Burundi, takribani mara mbili kwa Kenya, takribani mara nne kwa Uganda.
Hii siyo nchi ndogo hata kidogo. Kutoka kituo kimoja cha mechi kwenda kingine hufikia hadi kilomita 1000.
Fikiria safari ya kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma, kilomita zaidi ya 1000. Fikiria safari ya kutoka Ruangwa hadi Mbeya, kilomita zaidi ya 1000. Safari ya Arusha hadi Bukoba, kilomita zaidi ya 1000.
Hii ndio nchi yetu...ukubwa wa ardhi yetu ni baraka lakini tusipokuwa makini itageuka kuwa laana.
Ligi ikiendeshwa kwa namna ambavyo Rais wa TFF anasema, wachezaji watachoka sana. Ikumbukwe wachezaji wetu wa timu ya taifa wanacheza ligi hii hii.
Sisi sio nchi ambayo wachezaji wake wanatoka Ulaya, kama Morocco au Ivory Coast au Senegal. Ni ligi hii hii inayolipuliwa ndiyo itakayotoa wachezaji ambao watashiriki AFCON itakayoandaliwa hapa nchini. Kwa ratiba ya kuumizana kama hiyo, maana yake mashindano yatafika na kuwakuta wachezaji wetu wako hoi.
Kwanza watachoka na safari ndefu za kutoka kituo kimoja hadi kingine. Vyombo vya usafiri wanavyotumia ni vya kiwango cha chini sana kwa wanamichezo. Haya mabasi wanayopanda yanaumiza miguu na migongo kwenye safari ndefu.
Sasa wakishachoshwa na safari, wanakuja kuchoshwa na dakika tisini za misukosuko kwenye mechi. Pata picha kwa safari hizi ndefu na mechi hizi ngumu zinakuja kila baada ya siku tatu... wachezaji watakuwa kwenye hali gani mwisho wa msimu?
Haya yote yanakuja tukiwa kwenye ligi ambayo mifumo yetu ya tiba na lishe kwa wachezaji haiko vizuri sana. Kurudisha miili ya wachezaji katika hali ya kawaida kila baada ya mechi ni mtihani...hata barafu tu huwa tatizo.
Hizi timu ndogo zinapoenda mikoani kwenye mechi zao, wanachofanya ni kuwapa hela wachezaji wakale kwa mama lishe. Hivyo sivyo wanamichezo wanavyopaswa kula.
Sasa mtu anapata tiba ya chini ya kiwango ikiwemo kurudisha miili katika hali ya kawaida na anakula wali maharage kwa mama lishe, unadhani mwili wake utakuwa sawa sawa kwa kuwa na ratiba ya aina ya anayoisema Karia? Mpira ni mchezo unaotumia nguvu na akili. Kimojawapo kisipokuwa sawa sawa, huwezi kupata kilicho bora kutoka kwa mchezaji.
TFF itaiharakisha ligi ili kufikia malengo yao ya kumaliza msimu mapema, lakini baada ya hapo ni wao ndio watakaopata aibu pale Taifa Stars itakapokuwa inaboronga kwa uchovu kwenye AFCON.
Wakati akiongea, Karia ni kama alikuwa anabishana na watu fulani. Akasema hataki kusikia makocha, viongozi au wasemaji wa timu wakilalamikia uchovu kwa wachezaji. Sasa wasipolalamika watu hawa...atalalamika nani...huku si ndiyo kuzibana midomo mapema?
Hawa watu ndiyo wanaosimamia timu....wanaoendesha timu na ndiyo wanaowajibika mbele ya wamiliki wa timu na mashabiki wao.
Matokeo yasipopatikana kwa sababu ya uchovu, kwa nini wasilalamike?
Kwamba timu zisajili wachezaji arobaini...daaah. Hili haliwezi kuwa suluhisho.
TFF inasema tu kuhusu wachezaji arobaini. Sijui kama wamewaza kuhusu uchumi wa hizi timu. Sijui kama wamewaza kuhusu ugumu wa kocha kulisimamia kundi kubwa kama hili mazoezini?
Ligi kuu ya England (EPL) kwa mfano, timu zina wachezaji 25 tu....sisi tunaongeza hadi 40. Sheria za EPL zinazitaka klabu kutozidisha wachezaji 40...sisi tunalazimishana kusajili wachezaji 40.
Sawa, sisi tuna mazingira yetu na utamaduni wetu na wao wana vya kwao...lakini mambo muhimu kama uchumi na ufundi hayatofautiani.