Raila kuwaokolea Gor na mchango wa 15 milioni

Thursday November 18 2021
raila pic
By Sinda Matiko

GOR Mahia wameamka tena na masaibu yao ya kawaida. Kama ilivyo ibada, Gor wako msoto kinoma na leo wameandaa mchango wakilenga kuchangisha Sh15 milioni.
Fedha hizo, klabu inapania kuzitumia kwenye maandalizi ya mechi zao mbili za CAF Confederation Cup mkondo wa pili wa mchujo baadaye mwezi huu.
Mchango wa leo  utakuwa wa wageni waalikwa pekee  katika hoteli ya nyota tano ya Serena jijini Nairobi. Shughuli nzima itaongozwa  na mlezi wa klabu  ambaye pia ni kiongozi wa upinzani kisiasa Raila Odinga.
"Tunawarai mashabiki wetu wajitolee kwa moyo mmoja kwenye mchakato huu wa kuchangisha fedha. Na kwa kuwa sio kila mmoja ataweza kufika Serena, kuna Paybill yetu 350100 wanayoweza kuitumia kutoa mchango wao.  Fedha hizi tunazitegemea sana kwa ajili ya maandalizi ya michuano yetu miwili ijayo ya CAF. Tunawarai sana watusaidie sababu gharama za mechi hizi ni ghali mno na kukosa kushiriki inaweza kutupelekea kufungiwa na CAF na hiyo itakuwa hasara kubwa kwetu."  Mkurugenzi pale Gor Lordvick Aduda karai.
Gor wanakutana na AS Otoho d'Oyo kutoka Jamuhuri ya Kidemkorasia ya Congo Novemba 28 ugenini kabla ya kuwa wenyeji wa mechi ya marudiano mjini Nairobi, Disemba 5.
Mechi  ya nyumbani itachezewa katika uwanja wa Nyayo baada ya CAF kuondoa marufuku dhidi ya matumizi ya uwanja huo ikidai haikukidhi viwango vyake. Gor walikuwa tayari wameanza mchakato wa kuomba nchi jirani Tanzania ruhusa ya kutumia uwanja wao wa kitaifa wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Advertisement