Peres Jepchirchir: Kutoka kuuguza majeraha hadi kushinda medali ya dhahabu Tokyo
Muktasari:
- Baada ya kurejea kutoka kwenye jeraha, Jepchirchir aliteuliwa katika timu ya Kenya ya marathon kwa ajili ya Mashindano ya Dunia ya Riadha ya 2025 yaliyofanyika Tokyo kuanzia Septemba 13, 2025 hadi Septemba 21, 2025.
Bingwa wa dunia wa mbio za marathoni, Peres Jepchirchir, anasema mapumziko ya miezi miwili kutokana na jeraha la mguu aliyopata Aprili 2025, yalimfanya arejee uwanjani akiwa na hamu kubwa ya mafanikio, jambo lililomsaidia kushinda medali ya dhahabu kwenye Mashindano ya Dunia ya Riadha ya 2025 mjini Tokyo.
Baada ya kurejea kutoka kwenye jeraha, Jepchirchir aliteuliwa katika timu ya Kenya ya marathon kwa ajili ya Mashindano ya Dunia ya Riadha ya 2025 yaliyofanyika Tokyo kuanzia Septemba 13, 2025 hadi Septemba 21, 2025.
Akiwa na shauku kubwa ya kurejea kushindana baada ya kupona jeraha la kifundo cha mguu wa kulia, alikubali mwaliko huo bila kusita. Jeraha hilo pia lilimfanya kukosa Marathon ya London ya 2025 iliyofanyika Aprili 2025.
Jepchirchir alishinda taji la wanawake la mbio za marathon kwenye Michezo ya Olimpiki ya 2020 mjini Tokyo, lakini alimaliza katika nafasi ya 14 kwenye Michezo ya Olimpiki ya 2024 mjini Paris. Anasema kila mara hufurahia kuiwakilisha Kenya kwenye mashindano ya kimataifa na hakuwaza mara mbili alipoteuliwa kufanya hivyo.
Alipata jeraha hilo wiki mbili kabla ya Marathon ya London 2025. Wakati wa mazoezi, Jepchirchir alikanyaga jiwe na kuumia kifundo cha mguu. Daktari wake alimshauri apumzike kwa miezi miwili ili kuepuka kuumiza zaidi. Kwa uchungu, alitangaza kujiondoa kwenye mbio hizo na kuanza safari ya kupona.
“Nilichukua mapumziko ya miezi miwili baada ya kupata jeraha. Kwa juhudi kubwa, nilipona na kurejea mazoezini tena. Ilikuwa ni uamuzi mgumu lakini niliulazimika kuukubali na kufuata ushauri wa daktari,” amesema Jepchirchir katika kipindi cha SportOn cha NTV kinachoongozwa na Bernard Ndong na James Wokabi.
Mwanariadha huyo anayeishi Kapsabet, pia alikuwa amepata mwaliko wa kushiriki Marathon ya Berlin Septemba 2025, lakini baada ya kushauriana na meneja wake, Gianni Demadonna, aliamua kuwakilisha Kenya kwenye Mashindano ya Dunia ya Riadha 2025 ambayo yalikuwa mbio ngumu kwake zaidi.
“Nilikimbia na (mwanariadha wa Ethiopia) Tigst Assefa kwenye Marathon ya London mwaka jana, na ingawa nilishinda, nilijua ni mkali. Katika mashindano ya dunia, wengine wote walichoka tukabaki wawili tu mbele. Nilikuwa nimehifadhi nguvu kwa ajili ya sehemu ya mwisho ya mbio, na mimi huwa si mtu wa kukata tamaa. Kwa sababu kama nimekimbia zaidi ya saa mbili, kwa nini nishindwe mwishoni?” ameuliza kwa utani Jepchirchir.
Wakati wanariadha wengi hukaa kambini wakiwa na makocha wanaowasimamia, Jepchirchir ni tofauti. Hana kocha na hutumia tu mpango wa mazoezi anaofuata kwa nidhamu kubwa.
“Ilikuwa vigumu kwa meneja wangu kukubali kwamba sitaki kocha. Aliniambia kwamba kama mwanariadha wa marathon ningehitaji kocha kwa wakati fulani, lakini nikamwambia najisikia vizuri kuendelea kujifanyia mazoezi peke yangu,” amesema.
Anasema siri ya mafanikio yake ni mumewe Davies Ngeno, ambaye humsaidia sana wakati wa mazoezi marefu. Jepchirchir, mwenye umri wa miaka 32, alianza kukimbia kwa bahati baada ya kujiunga na kundi la wanariadha waliokuwa wakifanya mazoezi Kapsabet. Alivutiwa na mafanikio ya bingwa wa zamani wa New York Marathon, Mary Keitany, katika mbio kubwa za mjini.
Jepchirchir alivunja rekodi ya Keitany ya mbio za marathon za wanawake pekee kwenye Marathon ya London ya 2024 baada ya kumaliza kwa muda wa 2:16:16. Rekodi hiyo sasa imevunjwa na Assefa, aliyekimbia kwa 2:15:50 kwenye Marathon ya London ya 2025.
“Ninapanga kushiriki katika mashindano yote saba ya World Major Marathon. Tayari nimekimbia London na Boston, natumai kushiriki yale mengine hivi karibuni. Mwaka huu nitakimbia Marathon ya Valencia kwa kuwa nilikosa London mwezi Aprili na bado ninajihisi imara,” amesema mwanariadha huyo ambaye pia ameshinda mataji matatu ya Dunia ya nusu marathon.