Kocha Gor Mahia akubali lawama, afichua sababu za kupigwa 4-1
Muktasari:
- Kipigo hicho kimekuja zikibaki siku chache kabla ya kushuhudiwa Dabi ya Mashemeji ambapo Gor Mahia itaikaribisha AFC Leopards, wikiendi hii katika mwendelezo wa ligi hiyo.
JANA Jumanne Novemba 25, 2025, mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu ya Kenya, Gor Mahia iliduwazwa na vibonde wa ligi hiyo, APS Bomet kwa kupokea kichapo cha mabao 4-1, huku Kocha wa Gor Mahia, Charles Akonnor, akikiri lawama zote anapaswa kupewa yeye.
Kipigo hicho kimekuja zikibaki siku chache kabla ya kushuhudiwa Dabi ya Mashemeji ambapo Gor Mahia itaikaribisha AFC Leopards, wikiendi hii katika mwendelezo wa ligi hiyo.
Akizungumza baada ya mechi, Akonnor amesema: "Haikuwa siku nzuri. Hatukufanya vizuri katika maeneo mengi. Tulishuka kiwango baada ya kufunga bao. Hatukuwa na ukali wa kutosha. Mimi ndiye ninayewajibika kwa hilo, na tunaangalia kufanya maboresho."
Katika mechi hiyo, Akonnor, alifanya mabadiliko tisa kutoka kikosi kilichoshinda 1-0 dhidi ya Tusker Jumamosi iliyopita, akilenga kulinda nguvu kwa ajili ya Dabi ya Mashemeji wikiendi hii. Aliwaingiza mastaa wake kipindi cha pili, lakini mabadiliko hayo hayakuletea mabadiliko.
Kuhusu kufanya mabadiliko tisa kwenye kikosi, Akonnor ameongeza: "Niliona uchovu kwa baadhi ya wachezaji wetu kwenye mchezo uliopita. Tunacheza Jumamosi, Jumanne, kisha Jumamosi tena. Sikuwa na nia ya kuidharau Bomet, lakini nilihisi ni muda sahihi kuwapa nafasi wachezaji wengine na kuwaweka wengine freshi kwa dabi. Haikufanikiwa.
"Tutahitaji kufanya vizuri katika mchezo ujao na kupata matokeo mazuri."
Kwa upande wa kocha wa APS Bomet, Benedict Wanjala, amesema: "Tumekuwa tukicheza vizuri lakini matokeo hayaji. Tumekuwa tukitengeneza nafasi nyingi bila kuzitumia. Nimefurahi kuona tumetekeleza tuliyofanyia kazi mazoezini."
Hata hivyo, Wanjala amesema hawapaswi kujisahau kwa ushindi huo kwani mbele yao kuna mechi nyingine ngumu zinakuja.
"Hatuwezi kusherehekea sana. Mchezo umeisha na tuna mechi ngumu zinakuja. Tunaendelea kujenga kujiamini kwa sababu wengi wa wachezaji wetu ni wageni kwenye kiwango hiki," amesema.
Gor Mahia imekubali kipigo hicho kikiwa ni kikubwa zaidi kukipata katika ligi tangu ilipofungwa 3-0 na Posta Rangers Januari 2022. Licha ya kipigo, Gor Mahia imesalia kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 19.
Pia ushindi huo umeiondoa Bomet mkiani na kuipeleka nafasi ya 17 ikikusanya pointi nane.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Nyayo, ilishuhudiwa Hansel Ochieng’ akifunga mabao mawili na kutoa pasi mbili za mabao kwa APS Bomet iliyotoka nyuma na kupata ushindi huo wa kihistoria.
Gor Mahia ilionekana kuwa kwenye njia ya kupata ushindi mzuri baada ya mshambuliaji wao mpya kutoka Ghana, George Amonoo, kufunga bao la kuongoza dakika ya tano. Hata hivyo, Bomet ilipambana na kuingia mapumzikoni ikiwa mbele kwa mabao 2-1 baada ya Ochieng’ kufunga penalti dakika ya 40 kisha kuongeza la pili dakika ya 43.
Ochieng’ alikuwa karibu kufunga hat-trick, lakini mpira alioupiga uliguswa na Philip Wasai na kuingia wavuni dakika ya 76. Dakika ya 87, Ochieng’ alitoa pasi safi iliyomuwezesha Rodgers Kipkemoi kufunga bao la nne na kukamilisha ushindi wa pili wa msimu kwa Bomet.
Baada ya mechi, shujaa wa Bomet, Hansel Ochieng’, amesema amekuwa akifurahia zaidi kucheza dhidi ya Gor Mahia.
"Hakuna jipya kwangu kufunga dhidi ya Gor. Ni hisia nzuri. Ushindi mzuri kwetu na mchezo mzuri wa kuonesha ubora wetu," amesema.