Nairobi United yafichua siri ya kuichapa Etoile du Sahel
Muktasari:
- Oduor amesema, alimuomba Mungu ampe ujasiri kabla ya Nai Bois kushuka dimbani kwa mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya pili baada ya nyumbani kushinda 2-0.
Kipa wa Nairobi United, Kevin Oduor, amefichua namna kikosi hicho kilivyofanikiwa kuifunga Etoile Sportive du Sahel ya Tunisia, Jumapili iliyopita Oktoba 26, 2025 na kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2025–26 kwa mara ya kwanza.
Oduor amesema, alimuomba Mungu ampe ujasiri kabla ya Nai Bois kushuka dimbani kwa mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya pili baada ya nyumbani kushinda 2-0.
“Nilitarajia kelele na miale ya laser. Nilichofanya ni kumwomba Mungu anipe ujasiri wa kukabiliana na mazingira kama hayo,” Oduor ameviambia vyombo vya habari vya klabu hiyo Jumapili Oktoba 26, 2025 huko Sousse, Tunisia, baada ya Nairobi United kuwaondoa mabingwa wa zamani mara mbili wa Kombe la Shirikisho Afrika na kuwa klabu ya kwanza kutoka Kenya kufuzu hatua ya makundi ya michuano ya CAF katika msimu wake wa kwanza kushiriki.
Nairobi United ilishinda kwa mikwaju ya penalti 7–6, baada ya Etoile du Sahel kusawazisha jumla ya mabao kuwa 2–2 kufuatia ushindi wa 2–0 wa Nai Bois katika mechi ya kwanza. Timu hiyo sasa imehakikishiwa shilingi milioni 52 za Kenya (Sh994.8 milioni za Tanzania) kwa kufikia hatua hii.
Oduor alikuwa shujaa wa mabingwa wa Kombe la MozzartBet 2025, akihakikisha ushindi huo kupitia miguso yake miwili ya mwisho kwenye mpira, kwanza akiuokoa mkwaju wa penalti wa Cedrik Gbo kutoka Ivory Coast, kisha akifunga penalti ya ushindi akimhadaa kipa wa Tunisia, Sabri Ben Hassen.
“Wakati ule ulipofika, nilijua nilipaswa kuwa mtulivu na makini kwa sababu nililazimika kufunga. Nilibaki mtulivu na nikafanya nilichopaswa kufanya kwa ajili ya timu yangu,” amesema Oduor.
Oduor aliokoa penalti mbili licha ya mashabiki wa Etoile du Sahel kummulika usoni kwa miale ya laser. Uokoaji wake wa kwanza ulikuja dhidi ya Nassim Hnid, aliyepiga mkwaju wa kwanza wa timu hiyo ya Tunisia, kabla ya penalti sita zilizofuata za Etoile kuingia wavuni.
“Naona tunaweza kwenda mbali kadiri iwezekanavyo,” amesema, ingawa amesisitiza umuhimu wa kubaki wanyenyekevu licha ya mafanikio yao ya haraka.
Nairobi United ilipanda daraja kuingia Ligi Kuu ya Kenya mwezi Mei 2025, kisha mwezi Juni 2025 ikashinda Kombe la FKF katika fainali yake ya kwanza baada ya kushinda 2-1 dhidi ya Gor Mahia, klabu yenye mataji mengi zaidi ya michuano hiyo ikishinda mara 11.
Ushindi huo dhidi ya Gor Mahia ndio uliowapa nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika 2025–26, ambapo ushindi wao dhidi ya Etoile du Sahel uliendeleza hadithi yao ya kishujaa.
“Sasa tunarudisha nguvu kwenye mechi za ligi tukisubiri droo ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la CAF. Lazima tubaki wanyenyekevu na tusibeze ubora wa wapinzani wetu,” amesema Oduor.
Nahodha wa timu hiyo, John Onyango, pia ametoa maoni yake kuhusu mechi hiyo aliyoiita ngumu sana.
“Mazingira yalikuwa magumu, tulicheza chini ya taa, hali ambayo hatuizoei. Tulijua changamoto zilizokuwa mbele yetu, tukakubaliana kubaki makini. Tulicheza kama timu moja,” amesema Onyango.
Onyango pia ameongeza: “Tulijua tutateseka. Wengi wetu hawajawahi kucheza katika kiwango hicho, kwa hiyo tulijua wakati fulani tungeweza kuyumba. Lakini tulisisitiza kuwa na nguvu ya kiakili kwa sababu haijalishi nini kingetokea, tulilenga kufuzu hatua inayofuata.”
Ushindi wa Nairobi United ulikuwa ni mchezo wa 47 kwa timu ya Kenya kucheza Afrika Kaskazini. Katika mechi 46 zilizotangulia, klabu za Kenya zilikuwa zimepoteza 44, huku Gor Mahia ikitoka sare ya 2–2 dhidi ya Esperance Sportive de Tunis mwaka 1987 na ushindi wa 3–1 dhidi ya Al-Ahli Merowe ya Sudan mwaka 2021.
Baada ya kipindi cha kwanza kisicho na mabao, Etoile du Sahel ilifungua ukurasa wa mabao dakika ya 50 kupitia Mohamed Rayane Anane. Timu hiyo ya Tunisia iliendelea kushambulia lakini Oduor na safu yake ya ulinzi iliendelea kuwa imara hadi dakika ya 96, ambapo Ghofrane Naouali alisawazisha kwa kichwa kilichompita Oduor.
Hata hivyo, Nairobi United haikukata tamaa na ikaibuka mshindi kwa mikwaju ya penalti, ikionyesha uthabiti ambao Mkurugenzi wa Ufundi wa timu hiyo, Salim Ali, aliuelezea kama matokeo ya imani kubwa ndani ya kikosi.
“Imani na uimara wa kiakili ndivyo vilivyotupa matokeo haya. Imani hii imekuwepo muda mrefu, na ilitusaidia kuona mbali. Watu wengi walitupuuza baada ya droo dhidi ya Etoile du Sahel, lakini sisi hatukuwahi kupoteza imani na wachezaji wetu. Kile nilichoona kutoka kwa vijana hawa ni cha kipekee, sijawahi kuona kitu kama hiki,” amesema Ali.
Droo ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu 2025–26 itafanyika Novemba 3, 2025, huko Johannesburg, Afrika Kusini. Timu 16, ikiwemo Nairobi United, zitagawanywa katika makundi manne ya timu nne kila moja.
Timu nyingine zitakazoshiriki droo hiyo ni: Al Masry (Misri), AS Otoho (Congo-Brazzaville), Azam (Tanzania), CR Belouizdad (Algeria), Djoliba (Mali), Kaizer Chiefs (Afrika Kusini), Maniema Union (DR Congo), Olympic Safi (Morocco), San Pedro (Ivory Coast), Singida Black Stars (Tanzania), Stellenbosch (Afrika Kusini), USM Alger (Algeria), Wydad Casablanca (Morocco), Zamalek (Misri) na ZESCO United (Zambia).