Momanyi mrithi wa Mieno Tusker FC

WAKATI ikiendelea na mazoezi ya kujiwinda na msimu mpya wa Ligi Kuu ya Kenya hapa jijini Arusha timu ya Tusker FC imemtambulisha Charles Momanyi kuwa nahodha mpya wa kikosi hicho akichukua nafasi ya kiungo Humphrey Mieno ambaye amepewa 'thank you'.

Kuteuliwa kwa mlinzi huyo ambaye amedumu kwa misimu miwili tangu alipojoiunga  na timu hiyo msimu wa 2021/22 akitokea Gor Mahia FC,inatoa taswira ya kwamba kocha Robert Matano anaamini Momanyi ana sifa zote ambazo zinahitajika katika utimizaji wa majukumu.

Atasaidiwa na nyota wawili mlinda lango Brian Bwire pamoja na mlinzi Michael Kibwage ambao sasa watabeba jukumu la kuongoza wachezaji wenzao ili kupambana tena na kutwaa ubingwa wa FKF ambao msimu uliopita walinyanganywa na Gor Mahia kwa tofauti ya alama moja pekee.

Tusker ilimaliza msimu wa 2022/23 wa FKF katika nafasi ya pili kwa alama 69 huku Kogalo ikitwaa ubingwa kwa alama 70.Timu zote zikicheza mechi 34.

Momanyi ameiambia Mwanaspoti kwamba anafurahi kupata nafasi ya kuwa kiongozi wa wachezaji wenzake huku akiamini kila kitu kitakwenda sawa kutokana na namna ambavyo wanaheshimiana kama wachezaji.

“Tutashirikiana kwa pamoja ili tuone tunafika katika hatua gani lakini malengo makubwa ni kutwaa ubingwa”anasema Momanyi.

Akizungumzia mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya Ligi ambayo Tusker FC inaendelea nayo kwenye uwanja wa Agha Khan iliyoko Ngaramtoni nje kidogo la jiji la Arusha amesema kila kitu kiko sawa kama wachezaji wanaendelea na maandalizi kuona namna gani wanapata muunganiko baina ya wale wa zamani na nyota wapya ambao wamesajiliwa.

“Kuna wachezaji wapya wamekuja hivyo hatujazoena naamini katika maandalizi ya wiki moja kila kitu kitakuwa kwenye msitari na Ligi ikianza hatutakuwa na ugumu wowote”anasema Momanyi.

Ligi Kuu Kenya inatazamiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 26 mwaka huu ambapo siku hiyo Tusker FC itakuwa mgeni katika ukanda wa Pwani yani jijini Mombasa itakapomenyana na Bandari FC.