Modo: Kwa tizi hili, Wazito hawachomoki

KOCHA wa Bandari FC, Anthony ‘Modo’ Kimani, amesema anawaandaa vijana wake kwa mechi yao dhidi ya Wazito FC itakayochezwa Muhoroni wikendi hii lengo likiwa ni kuondoka na pointi tatu.

Kimani alisema Wazito ni timu ngumu ukilinganisha na Kakamega Homeboyz FC ambayo Bandari FC ilipata ushindi dhidi yao katikati ya wiki iliyopita hivyo ndio maana anatekeleza mikakati ya kujitayarisha ili kuibuka na ushindi.

“Tunahitaji alama tatu ili tupate kusonga juu katika ngazi ya ligi kwani tungali sehemu ambayo hatustahili kuwako,” alisema Kimani.

Mkufunzi huyo alisema ushindi ambao vijana wake waliupata dhidi ya Homeboyz umewapa motisha kufanya vizuri zaidi kwenye mechi zao zijazo.

“Tunaamini tuna uwezo wa kuwa miongoni mwa klabu bora na ndio maana tunaendelea kuwanoa vijana waweze kutinga mabao katika kila mechi. Tunataka kuondoa tatizo la kupata nafasi na kuzipoteza,” alisema Kimani.