Mnigeria aing'oa Polisi Kenya, tumaini limebaki kwa Nairobi United
Muktasari:
- Polisi inayonolewa na kocha Mrundi, Etienne Ndayiragije ilifumuliwa kwa mabao 3-1 jana Ijumaa kwenye Uwanja wa Benina Martyrs, huko Libya na kutolewa kwa kipigo cha jumla cha 4-1.
MABAO mawili yaliyowekwa kimiani na straika Mnigeria, Sunday Adetunji anayekipiga Al Hilal ya Sudan yametosha kuing'oa Polisi Kenya katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Polisi inayonolewa na kocha Mrundi, Etienne Ndayiragije ilifumuliwa kwa mabao 3-1 jana Ijumaa kwenye Uwanja wa Benina Martyrs, huko Libya na kutolewa kwa kipigo cha jumla cha 4-1.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Kenya awali ililambwa bao 1-0 ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Ulinzi Sports Complex, jijini Nairobi wikiendi iliyopita.
Wenyeji waliohamia Libya kwa sasa kutoka Mauritania ilipokuwa msimu uliopita kutokana na machafuko ya kisiasa huko Sudan, iliandika bao la kwanza dakika ya 37 kupitia Adetunji lilodumu hadi mapumziko.
Hata hivyo, kipindi cha pili kilipoanza Polisi ilichomoa bao hilo dakika ya 53 likifungwa na Erick Zakayo, lakini dakika 11 baadae Adeyunji alipigilia msumari wa pili kwa wenyeji.
Bao la tatu ya Al Hilal iliyofuzu makundi kwa mara nyingine ikiungana na Azam FC ya Tanzania, CR Belouizdad ya Algeria na Wydad Casablanca ya Morocco lilifungwa dakika 11 za nyongeza za pambano hilo kupitia Ahmed Salem.
Matokeo hayo yameifanya mashabiki wa Kenya kwa sasa kuweka tumaini la kuingiza timu katika makundi kupitia Nairobi United.
NaiBoyz ilipata ushindi wa kushangaza wikiendi iliyopita kwa kuichapa Etoile du Sahel ya Tunisia mabao 2-0 jijini Nairobi.
Wawakilishi hao wa Kenya watashuka uwanjani kesho Jumapili ikiwa ugenini ikihitaji sare yoyote kuifuata nyayo za Gor Mahia iliyokuwa ya mwisho kucheza makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika misimu miwili mfululizo mwaka 2018 na 2018-2019 ilipotolewa robo fainali ya RS Berkane ya Morocco kwa jumla ya mabao 7-1
Mechi hiyo ya Etoile du Sahel na Nairobi United inatarajiwa kupigwa kuanzia saa 2:00 usiku kwenye Uwanja wa Olympique de Sousse, jijjini Sousse, Tunisia ukiwa ndio uwanja wa mabingwa hao wa zamani wa Afrika.
Al Hilal imeingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya 14 msimu huu.
Lakini ni mara ya saba mfululizo kwa wababe hao wa Sudan ikiwa ni nyuma ya Al Ahly ya Misri iliyoingia mara 10, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini pia mara 10 na Esperance ya Tunisia mara 9 mfululizo.