Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mkenya Chepngetich aendelea kushikilia rekodi ya dunia licha ya kifungo

Muktasari:

  • Chepngetich alivunja rekodi hiyo mjini Chicago, Marekani Oktoba mwaka jana, kabla ya  kusimamishwa kwa muda Julai mwaka huu na Kitengo cha Maadili cha Riadha (AIU) baada ya sampuli yake ya damu iliyochukuliwa Machi 14 kugundulika kuwa na Hydrochlorothiazide (HCTZ), ambayo ni dawa inayotumika kutibu uvimbe wa maji mwilini na shinikizo la damu.

MKENYA anayeshikilia rekodi ya dunia ya mbio za marathoni kwa wanawake, Ruth Chepngetich, aliyefungiwa miaka mitatu baada ya kukiri kukiuka kanuni za kupinga matumizi ya dawa za kusisimua misuli (doping), bado muda wake wa 2:09:56 utaendelea kutambulika, kwani uliwekwa kabla ya kupatikana na kosa hilo.

Chepngetich alivunja rekodi hiyo mjini Chicago, Marekani Oktoba mwaka jana, kabla ya  kusimamishwa kwa muda Julai mwaka huu na Kitengo cha Maadili cha Riadha (AIU) baada ya sampuli yake ya damu iliyochukuliwa Machi 14 kugundulika kuwa na Hydrochlorothiazide (HCTZ), ambayo ni dawa inayotumika kutibu uvimbe wa maji mwilini na shinikizo la damu.

Sampuli hiyo ilionyesha kiwango cha 3,800ng/mL cha HCTZ, ambacho kiko juu ukilinganisha na kiwango cha chini kinachoruhusiwa na Wakala wa Dunia wa Kupambana na Doping (WADA) ambacho ni 20ng/mL.

Hapo awali, Chepngetich alikanusha makosa hayo na kushindwa kueleza chanzo cha matokeo hayo, hata baada ya uchunguzi wa kina wa AIU ulioshirikisha uchambuzi wa dawa, virutubisho na data ya simu yake.

Hata hivyo, Chepngetich alibadili maelezo kuhusu matokeo ya uchunguzi Julai 31, wiki mbili baada ya kusimamishwa, kwa kudai alimeza kwa bahati mbaya dawa za mfanyakazi wake wa nyumbani zilizokuwa na HCTZ alipokuwa mgonjwa.

AIU ilieleza kuwa, HCTZ hutumika kutibu uvimbe na shinikizo la damu, lakini inaweza pia kutumiwa kuficha uwepo wa dawa nyingine haramu mwilini.

AIU ilisema vitendo vya Chepngetich vilikuwa vya uzembe na vya makusudi kwa kiasi fulani na awali walipendekeza adhabu ya miaka minne.

Hata hivyo, kukiri kwake mapema kulipunguza adhabu hiyo kwa mwaka mmoja, hivyo akapewa kifungo cha miaka mitatu kuanzia Septemba 10.

Kiongozi wa AIU, Brett Clothier, alisema;
“Kesi kuhusu kipimo chanya cha HCTZ imekamilika, lakini AIU itaendelea kuchunguza nyenzo zilizopatikana katika simu ya Chepngetich ili kubaini kama kuna ukiukaji mwingine wowote.”

“Kwa sasa, mafanikio na rekodi zote za Chepngetich zilizowekwa kabla ya tarehe Machi 14, 2025 zitasalia kutambulika.”

Shirika la habari Reuters lilikaririwa likisema limewasiliana na wawakilishi wa Chepngetich kwa maoni zaidi.

Mapema Aprili, Chepngetich alijiondoa katika mbio za London Marathon, akisema hakuwa katika hali nzuri kiakili wala kimwili kushindana, ingawa ukweli ni kwamba alikuwa ameamua kusitisha mashindano kwa hiari wakati huo.

Mchezo wa marathon umeathiriwa sana na visa vya doping miaka ya hivi karibuni, hasa nchini Kenya, ambayo inatambulika duniani kwa wakimbiaji wake wa masafa ya kati na marefu.

Mnamo Novemba 2022, Kenya iliepuka kufungiwa licha ya idadi kubwa ya wanariadha wake kusimamishwa kwa makosa ya doping.

Shirikisho la Riadha Kenya (Athletics Kenya) lilisema serikali iliahidi kutoa dola 5 milioni  kwa mwaka kwa kipindi cha miaka 5 kusaidia mapambano dhidi ya doping.

Mnamo Februari 2024, Sarah Chepchirchir pia wa Kenya alifungiwa miaka 8 baada ya kupatikana na makosa ya doping kwa mara ya pili, alipogunduliwa kuwa na testosterone mwilini.

Mapema mwaka huu, Brimin Kipkorir, mshindi wa Sydney Marathon 2024 kwa rekodi ya muda wa mbio hizo, pia alisimamishwa kwa muda baada ya kupatikana na dawa zilizopigwa marufuku.