Nairobi United yawazima mabingwa wa zamani wa CAF
Muktasari:
- Nairobi United ilipata ushindi huo katika mechi ya mkondo wa kwanza wa raundi ya pili ya michuano hiyo ya CAF iliyopigwa kwenye Uwanja wa Ulinzi Sports Complex, jijini Nairobi Kenya.
WAWAKILISHI wa Kenya katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Nairobi United jioni hii imewaduwaza mabingwa wa zamani wa Afrika, Etoile du Sahel ya Tunisia kwa kuichapa mabao 2-0.
Nairobi United ilipata ushindi huo katika mechi ya mkondo wa kwanza wa raundi ya pili ya michuano hiyo ya CAF iliyopigwa kwenye Uwanja wa Ulinzi Sports Complex, jijini Nairobi Kenya.
Mabao mawili yaliyowekwa kila moja katika kipindi kimoja cha mechi hiyo kiliizima vigogo hivyo vya Tunisia, wanaorudi nyumbani kujiuliza wikiendi ijayo ili kuamua hatma ya kutinga makundi au la.
Etoile du Sahel imewahi kuwa bingwa Ligi ya Mabingwa Afrika 2007, pia imebeba Kombe la Shirkisho Afrika 2006 na 2015 mbali na mataji mawili ya Kombe la Washindi Afrika 1997, na 2003 pamoja na mawili ya Kombe la CAF 1995, na 1999,pia ikibeba CAF Super Cup 1998 na 2008.
Michuano ya Kombe la Washindi na CAF ndio yaliyounganishwa mwaka 2004 na kuzaliwa Kombe la Shirikisho.
Bao la kwanza la 'Naibois' liliwekwa wavuni dakika ya 37 kaa kichwa na Ovella Ochieng na kudumu hadi mapumziko kabla ya kuongeza la pili dakila ya 52.
Naiboi ilitinga hatua hiyo baada ya kuing'oa NEC FC ya Uganda kwa faida ya bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya 3-3, ikianza na sare ya 2-2 ugenini jijini Kampala na kutoka 1-1 jijini Nairobi na sasa inahitaji sare yoyote ugenini wikiendi ijayo kuandika rekodi ya kutinga makundi kwa mara ya kwanza kwa timu hiyo kufuata nyayo za Gor Mahia iliyocheza mwaka 2018.