Mjukuu wa Kipchoge ang’ara Africa Duathlon Cup
Muktasari:
- Duathlon ni mchezo wa mseto unaojumuisha vipengele vitatu: kukimbia, kuendesha baiskeli, na kumalizia tena kwa kukimbia. Ni sawa na triathlon, lakini bila kipengele cha kuogelea.
Mwanariadha chipukizi, Joseph Okal ambaye ni mjukuu wa gwiji wa riadha, Kipchoge Keino, ameendeleza urithi wa familia kwa kutwaa ushindi katika mbio za wanaume wa daraja la juu (Elite Men) za Africa Duathlon Cup zilizofanyika mjini Kilifi mwishoni mwa wiki.
Katika mashindano hayo yaliyoandaliwa Jumamosi, Oktoba 13, 2025, Okal alimaliza mbio hizo kwa muda wa 1:03:14, akipambana katika hali ya hewa ya joto na unyevunyevu. Baada ya ushindi wake, Okal mwenye umri wa miaka 25, alitaja mafanikio yake kuwa yalichangiwa zaidi na ubora wa mabadiliko kutoka baiskeli hadi kukimbia, nguvu ya kiakili, na uvumilivu wa mwili.
“Nilikuwa na mabadiliko ya haraka sana, nikaweza kuwafikia wenzangu kisha nikaongeza kasi. Mafanikio yangu leo yametokana na maandalizi mazuri hasa kwa upande wa mabadiliko,” amesema Okal, ambaye hufanya mazoezi katika shamba la Kazi Mingi huko Eldoret.
“Funzo langu kubwa ni kuwa maendeleo huja kulingana na bidii yako. Mafanikio unayovuna ni matokeo ya juhudi unazoweka. Wakati fulani haikuwa tena suala la muda, bali nguvu ya kiakili,” ameongeza.
Duathlon ni mchezo wa mseto unaojumuisha vipengele vitatu: kukimbia, kuendesha baiskeli, na kumalizia tena kwa kukimbia. Ni sawa na triathlon, lakini bila kipengele cha kuogelea.
Okal tayari amewahi kuiwakilisha Kenya kwenye Mashindano ya Jumuiya ya Madola (Commonwealth Games) mwaka 2022 huko Birmingham, akishiriki katika triathlon.
Katika mbio hizo, Okal ameongoza kuanzia mabadiliko ya kwanza hadi akamalizia sehemu ya mwisho ya mbio kwa muda wa dakika 38 na sekunde 1.
Nafasi ya pili ilichukuliwa na Lewis Kinyua aliyemaliza kwa 01:03:24, huku David Wanjiru akishika nafasi ya tatu kwa muda wa 01:04:39.
Kinyua alieleza kuwa mashindano hayo kwake yalikuwa ya kujifunza.
“Nilipoteza muda mwingi kwenye mabadiliko, lakini kwa uzoefu tutazidi kuboresha. Njia haikuwa rahisi na barabara ilikuwa na mashimo, lakini niliendelea. Mbio fupi ni ngumu zaidi kwa sababu nimezoea mbio ndefu. Lengo langu ni kufikia viwango vya dunia,” amesema.
Kwa upande wa wanawake, Megan Irungu ameibuka mshindi wa mbio za Elite Women, akimaliza kwa muda wa 01:13:56. Nafasi ya pili imeenda kwa Bernice Kariuki (01:19:07), naye Adell Wamalwa akamaliza wa tatu kwa 01:29:04 baada ya pambano kali dhidi ya Iman Kaiza, aliyeshika nafasi ya nne kwa 01:35:20.
Kocha msaidizi wa timu ya taifa ya duathlon, Alphan Mwanyika, amefurahishwa na kiwango cha juu cha vipaji vilivyojitokeza, akiomba serikali na wadau kuongeza uwekezaji katika mchezo huo.
“Mchezo huu unakua kwa kasi. Tukijumuisha mazoezi bora, lishe nzuri, na kujenga miundombinu inayohitajika, tutaweza kuwakilisha nchi vyema kimataifa,” amesema.
Rais wa Triathlon Kenya, Joyceline Nyambura, amesisitiza umuhimu wa kuandaa mashindano makubwa nchini humo ili kuwapa wanariadha wa Kenya fursa ya kujipatia pointi za viwango vya kimataifa bila kusafiri nje.
“Wachezaji wetu walifanya vyema sana, hasa waliopanda jukwaani. Tunashukuru serikali kwa kutuunga mkono kuandaa mashindano hapa nchini, jambo ambalo linasaidia wanariadha wetu kupata pointi nyumbani. Kama shirikisho, tunalenga kukuza mchezo huu kuanzia ngazi ya chini na kuutambulisha zaidi mashuleni,” ameongeza.
Matokeo ya Africa Duathlon Cup – Kilifi 2025
Wanaume
Joseph Okal – 01:03:14
Lewis Phineas – 01:03:24
David Wanjiru – 01:04:39
Hamza Bashir – 01:06:07
Wanawake
Megan Irungu – 01:13:56
Bernice Kariuki – 01:19:07
Adell Wamalwa – 01:29:04
Iman Kaiza – 01:35:20