Masaibu yaiandama Gor Mahia

TABIA ya uongozi wa Gor Mahia kuendelea kuwatimua wachezaji wake pasi na kuzingatia utaratibu wa mikataba, unazidi kuwatia kwenye ngori.

Sasa tena kipa kutoka Mali, Adama Keita waliyemtimua hivi majuzi, amewashataki kwa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), akidai kuvunjiwa mkataba wake na miamba hao wa soka nchini bila ya utaratibu kufuatwa. Aidha Adama kadai kando na hilo, Gor wamedinda kumlipa mshahara wake.

Keita aliyafikisha malalamishi yake FIFA kuelekea mwisho wa msimu uliopita 2021/22 baada ya klabu kukosa kumlipa stahiki zake zote kama walivyokubaliana kwenye mkataba waliotia saini.

Kuelekea mechi za mwisho wa msimu huo, Adama alirushwa benchi kabla ya kutimuliwa wiki iliyopita pamoja na straika kutoka Congo, Yangayay Sando.

“Nilisaini mkataba wa miaka miwili nao na wameikiuka hata zaidi kwa uamuzi wa kunifukuza. Ombi langu kwao ni moja tu, wanilipe fedha ninazowadai tumalizane. Sitaki tuvutane lakini kama ikilazimu basi nipo tayari. Wamekuwa wakinizungusha sana na nimechoka sasa,” alilalamika Adama.

Gor ilimsaini Adama mwanzoni mwa msimu wa 2021/2022 kutoka CL Kamsar ya kule Guinea.

Usajili wake ulizua utata huku kukizuka madai kwamba hakusajiliwa kutokana na ubora wake ila alisajiliwa kwa ajili ya kuwafaidi baadhi ya makateli ndani ya klabu hiyo.

Hata hivyo Gor ilitetea hatua yake kwa kusema kipa huyo alipendekezwa na kocha Mark Harrison aliyetimuliwa Januari 2022, baada ya miezi sita tu tangu kuteuliwa.

Kushtakiwa tena FIFA huenda kukawaweka pabaya hata zaidi Gor ukizingatia Novemba mwaka jana walifungiwa na chombo hicho kufanya usajili.

Marufuku hiyo ilitokana na Gor kushindwa kuwafidia beki Mganda Shafik Batambuze, wing’a Mtanzania Dickson Ambundo na kocha Steven Polack, walioishtaki klabu hiyo FIFA kwa kuvunjiwa mikataba pasi na utaratibu unaostahili kufuatwa.

FIFA iliwakuta Gor na hatia na kuwaamuru wawafidie watatu hao zaidi ya Sh10 milioni kwa ujumla. Baada ya makataa waliyopewa kupita bila kutimiza amri hiyo, FIFA iliwafungia K’Ogalo kufanya usajili hadi 2023.

Kutokana na marufuku hiyo, Gor imeamua kubusti kikosi chake cha msimu ujao kwa kuwapromoti wachezaji kutoka kwa kikosi chao cha chipukizi.