Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo matatu mkutano wa Kipchoge na Obama Marekani

Muktasari:

  • Katika mkutano huo uliofanyika Washington, Marekani, Kipchoge alieleza dhamira yake ya kuhamasisha na kuwawezesha vijana kupitia michezo, elimu na uongozi.

Bingwa mara mbili wa Olimpiki katika mbio za marathon, Eliud Kipchoge, baada ya kumaliza kushiriki New York Marathon, Ijumaa Novemba 7, 2025 alikutana na Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, kujadili kuhusu nguvu ya mabadiliko inayotokana na michezo. Katika majadiliano hayo, mambo makuu matatu yaliwekwa mezani.

Katika mkutano huo uliofanyika Washington, Marekani, Kipchoge alieleza dhamira yake ya kuhamasisha na kuwawezesha vijana kupitia michezo, elimu na uongozi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wasimamizi wake, Global Sports Communications, Kipchoge amesema anamthamini sana Obama, akimtaja kama mtetezi wa amani na umoja duniani, ambaye amebaki mnyenyekevu na mwenye nidhamu katika maisha yake yote, thamani ambayo pia inaakisi maisha ya Kipchoge.

“Kukutana na Rais Obama ni tukio nitakalolikumbuka milele. Imenipa nguvu zaidi ya kuendelea kuhamasisha wale walioko karibu nami tunapojitahidi kuelekea dunia yenye umoja,” amesema Kipchoge.

Katika mazungumzo hayo, Kipchoge na Obama, ambao wote ni viongozi kwa nafasi zao, walijadili kwa kina kuhusu uongozi, urithi na jukumu muhimu la vijana katika kuunda mustakabali wa dunia.

“Mazungumzo yetu yalikuwa ya kutafakari na kushirikiana mawazo kuhusu uongozi, urithi, na namna kizazi kijacho kinaweza kuinuka kupitia michezo, elimu na huduma kwa jamii,” ameongeza Kipchoge.

Wote wawili walijadili uwezekano wa ushirikiano kati ya taasisi mbili za Eliud Kipchoge Foundation na Obama Foundation.

Mashirika hayo yanakusudia kukuza uongozi wa vijana, kupanua fursa za elimu, na kutumia nguvu ya michezo kubadilisha maisha ya vijana ili waamini kuwa hakuna ndoto iliyo mbali sana na hakuna mwanzo ulio mdogo.

“Tunashirikiana katika maono ya matumaini na uwezekano, tukiamini kuwa kupitia ushirikiano tunaweza kuleta mabadiliko yenye maana,” amesema Kipchoge, ambaye alimaliza mbio za New York Marathon Novemba 2, 2025 akiwa nafasi ya 17.

Kwa upande wake, Rais Obama alimshukuru Kipchoge kupitia ukurasa wake wa Instagram, akiandika: “Asante kwa maneno hayo mazuri. Ilikuwa vizuri sana kukutana nawe, Eliud!”

Kipchoge sasa amekamilisha mbio zote saba za Abbott World Marathon Majors (WMM), mafanikio adimu yanayothibitisha urithi wake katika riadha ambayo ameihusudu kwa zaidi ya muongo mmoja.

Baada ya kumaliza mbio hizo, Kipchoge alikabidhiwa medali za kukamilisha mashindano makuu sita ambayo ni Tokyo, Boston, London, Berlin, Chicago, na New York Marathon.

Mnamo Agosti 30, 2025, Kipchoge alishiriki Sydney Marathon, ambayo mwaka huu ilijumuishwa kwa mara ya kwanza kwenye orodha ya WMM, na alimaliza katika nafasi ya tisa.

Kwa mwanariadha ambaye amevunja vizingiti vingi ikiwemo kuwa mtu wa kwanza duniani kukimbia marathon chini ya saa mbili, ushiriki wake katika mbio sasa una maana kubwa sawa na ushindi.

Baada ya kumaliza mbio za New York, Novemba 2, 2025 Kipchoge alitangaza hatua mpya katika taaluma yake ya riadha alipoandika kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii: “Marathon saba katika mabara yote saba, pamoja nanyi! Kupitia World Tour hii, nataka kuendelea kujisukuma kufikia kiwango changu bora zaidi, lakini pia nataka kuhamasisha, kurudisha kwa jamii na kuwakumbusha watu wote kuwa hakuna binadamu aliye na mipaka kila kona ya dunia. Naamini tunaweza kuungana na kuufanya ulimwengu kuwa bora zaidi.”.

Kipchoge anachukuliwa na wengi kuwa mwanariadha bora zaidi wa marathon wa muda wote.

Tangu alipoanza kukimbia mbio za marathon katika Hamburg Marathon mwaka 2013, amekuwa akitawala mbio hizo duniani, akishinda medali mbili za dhahabu za Olimpiki (Tokyo 2020 na Paris 2024).

Kati ya mbio kuu 17 alizoshiriki, ameshinda 12, zikiwemo mara nne London Marathon na mara tano Berlin Marathon.

Mnamo mwaka 2019 huko Vienna, Kipchoge alikimbia chini ya saa mbili (1:59:40) katika mashindano maalum ya INEOS 1:59 Challenge, akawa binadamu wa kwanza kufanikisha hilo.

Pia aliweka rekodi ya dunia mara mbili katika Berlin Marathon, kwanza mwaka 2018 (2:01:39), kisha akaiboresha tena mwaka 2022 (2:01:09).

Baadaye, marehemu Kelvin Kiptum aliivunja rekodi hiyo kwa muda wa 2:00:35 katika Chicago Marathon, na kuwa mtu wa kwanza kukimbia kilomita 42 chini ya saa mbili na dakika mbili.