Kumekucha Bandari, Mathare

UONGOZI wa Bandari FC na Mathare United umefanya mabadiliko kwenye mabenchi yao ya ufundi kwa lengo la kunusuru timu zao katika mechi za Ligi Kuu Kenya zilizosalia.

Bandari FC imefikia makubaliano ya kuachana na kocha wake, Anthony ‘Modo’ Kimani, kufuatia timu hiyo kutolewa michuano ya Kombe la FKF hatua ya robo fainali.

Bandari FC ilichezea kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa AFC Leopards na kabla ya mechi hiyo ya Mozzart Bet Cup ilikua imefunga kwa idadi hiyo hiyo ya mabao dhidi ya Kenya Police FC.

Katika taarifa iliyomnukuu Katibu Mtendaji wa Bandari FC, Edward Oduor, Bodi ya Wadhamini wa klabu hiyo na kocha Kimani walifikia makubaliano ya kuachana.

“Tungependa kumshukuru Kimani kwa huduma yake na kujitolea kwa klabu wakati wa uongozi wake kama kocha mkuu wetu na tunamtakia kila la kheri katika mipango yake ya siku za usoni,” ilisomeka taarifa hiyo.

Taarifa ya Oduor ilimtangaza Mkurugenzi wa Ufundi wa Bandari FC, Sheikh Twahir Muhiddin, kuchukua mikoba ya Kimani kwa mechi zilizosalia.

Wakati huo huo, Mathare United imemteua Collins ‘Korea’ Omondi kocha mkuu mpya akichukua mikoba ya Samuel Koko aliyekua akikaimu na sasa anarudi kwenye majukumu yake yake ya ukocha wa makipa.

Mbali na kumteua Omondi, Mathare United pia imemrudisha kundini aliyekua kocha wa Wazito FC na Posta Rangers, Stanley Okumbi, ambaye anakua mkurugenzi wa ufundi.

Okumbi na Omondi wanakutana tena baada ya kufanya kazi pamoja wakiwa Posta Rangers ambapo Okumbi alikua kocha mkuu na Omondi msaidizi wake.