Kocha wa Congo Boys akacha wanahabari

Tuesday August 10 2021
By Abdulrahman Sheriff

KOCHA wa Congo Boys FC, Abdunassir Kassim alishindwa kuongea na wanahabari mwishoni mwa mechi yao ya Ligi ya Kitaifa Daraja ya Kwanza baada ya kupokea kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Zetech Titans FC.
Katika mchezo huo uliofanyika uwanja wa Serani Sports juzi Jumamosi, Kassim hakuamini kama atapoteza mechi hiyo kwani iliwachukua dakika tano za mchezo kuanza kupata bao la kuongoza lilotingwa nyavuni na Issa Adim kupitia mkwaju wa penalti.
Lakini bao hilo halikumudu muda mrefu kwani dakika nne baaadaye, Zetech iliweza kusawazisha kupitia kwa Austin Ochieng. Wageni hao waliweza kujipatia bao la pili dakika ya 12 mfungaji akiwa Prince Ila. Joel Shibunji alitinga nyavu bao la tatu kwenye dakika ya 90.
Kocha Kassim alipojongelewa na wanahabari kutaka azungumze juu ya matokeo hayo na kama timu itaweza kujinasua kutoka kuteremshwa ngazi na kubakia ligi hiyo, alionyesha huzuni akisema timu imerudi tena nafasi mbaya na hangependa kuzungumza lolote.
Kocha wa Zetech Titans, Bernard Chitolo anasema timu yake ilikuja Mombasa ikiwa imejipanga kuzoa pointi zote tatu huku akiwashauri wachezaji wake wajihadhari dakika za mwanzo sababu alifahamu Congo watadhamiria kupata bao la haraka.
“Ninawapongeza wachezaji wangu kwa kuwa watulivu hata baada ya Congo kupata penalti ambayo siamini kama ilikuwa halali dakika ya tano, wakaweza kusawazisha haraka na kupata bao la pili kabla ya dakika 15 za mwanzo hivyo nilitambua ushindi uko,” akasema Chitolo.
Congo imebakisha mechi tano mbili dhidi ya wenzao wa Pwani, SS Assad FC ya Ukunda ambayo iko nafasi ya pili katika jedwali na kuwa na tamaa ya kupanda hadi Ligi ya Kitaifa ya Supa (Supaligi) na Young Bulls FC ya Malindi ambayo nayo ingali hatarini kuteremshwa ngazi.

Advertisement