Kocha Nairobi United: Tuna mlima mrefu wa kupanda CAF
Muktasari:
- Nairobi United inayoiwakilisha Kenya katika Kombe la Shirikisho Afrika ikipangwa Kundi B, jana Jumapili Novemba 30, 2025 ilipoteza kwa bao 1-0 nyumbani dhidi ya AS Maniema Union kutoka DR Congo, mechi ikichezwa Uwanja wa Moi Kasarani.
BAADA ya kusubiri kwa miaka sita kushuhudia timu ya Kenya inacheza mechi ya nyumbani katika michuano ya CAF hatua ya makundi, hatimaye subira hiyo imekuja na maumivu huku kocha wa Nairobi United, Salim Ali akibainisha wazi kwamba wana mlima mrefu wa kupanda ili kufuzu robo fainali.
Nairobi United inayoiwakilisha Kenya katika Kombe la Shirikisho Afrika ikipangwa Kundi B, jana Jumapili Novemba 30, 2025 ilipoteza kwa bao 1-0 nyumbani dhidi ya AS Maniema Union kutoka DR Congo, mechi ikichezwa Uwanja wa Moi Kasarani.
Baada ya mechi hiyo ambayo ni ya pili kwa Nairobi United kupoteza hatua ya makundi msimu huu, kocha wa kikosi hicho, Salim Ali, ameonyesha majuto akisema: “Tumepoteza pointi tatu dhidi ya timu ambayo ingeweza kufungika.”
“Katika kipindi cha pili tulipoteza umakini na Maniema walitumia nafasi yao. Kiufundi walicheza vizuri. Ni timu yenye uzoefu na waliudhibiti mchezo. Walifanya kipindi cha pili kiwe kigumu kwa kupoteza muda.”
Kuhusu mipango ya kutafuta nafuu baada ya kichapo hicho, Ali amesema: “Baada ya kupoteza pointi sita, tuna mlima mrefu wa kupanda. Tuna mechi nne mbele yetu, lazima tuzishinde zote.”
Kocha wa Maniema, Papy Kimoto, amesema mechi ilikwenda kama walivyopanga: “Tunafurahi kupata pointi tatu, lakini tunahitaji kufanya kazi zaidi.”
Bao la Maniema lilifungwa na mchezaji wa akiba, Jeancy Mboma, dakika ya 65, likiwa ni shuti pekee la timu hiyo lililolenga goli la wapinzani.
Kocha Kimoto ameelezea bao hilo akisema: “Tulipaswa kusubiri wakati wetu ufike. Tuliwaacha Nairobi United washambulie kisha tukawashinikiza kwa wakati sahihi ili tufungue mianya ya kushambulia kwa kasi.”
Mechi hiyo ilianza kwa Nairobi United licha ya kumiliki mpira katika dakika tano za kwanza, pasi mbaya ilimruhusu Obed Mbala kupiga shuti nje baada ya kutengenezewa na Christian Balako.
Baadaye, Balako alipiga shuti nje dakika ya 20 baada ya pasi nyingine iliyopotezwa kumpa nafasi Clement Pitroipa kutengeneza nafasi hiyo.
Hata hivyo, Nairobi United ilionyesha viashiria vya matumaini kupitia safu ya ushambuliaji iliyojumuisha Dancan Omalla, Enock Machaka, Michael Karamor na Shami Kibwana.
Karamor alipiga nje dakika ya 11, kisha akakosa kuunganisha krosi ya Machaka dakika ya 25.
Omalla alipiga shuti lililogonga pembeni ya wavu dakika ya 12 na lingine nje dakika ya 26. Kibwana, mchezaji aliyekuwa na umri mkubwa zaidi uwanjani siku hiyo, alipiga mpira wa adhabu moja kwa moja uliotua mikononi mwa Detan Ogundare dakika ya 36.
Kipindi cha pili kilirejea kwa pambano la kubadilishana mashambulizi. Kila upande ulizima mashambulizi ya mwenzake kwa kuingilia kwa wakati na makosa yaliyosababisha krosi na kona zisizo na madhara.
Dakika ya 65 mambo yalibadilika. Shambulizi la kasi la Maniema lilimfungua mchezaji wa akiba, Jeancy Mboma, aliyeingia dakika ya 46. Mboma alikimbia na mpira kwenye upande wa kushoto, akaingia ndani ya boksi kisha akampigia Kevin Oduor shuti la chini lililopita kwenye mwamba wa karibu.
Nairobi United ilijibu kwa kufanya mabadiliko matatu, Brian Mogire, Dancan Omalla na Enock Machaka wakatoka nafasi zao kuchukuliwa na Adams Nyambane, Kefa Nakhumicha na Chris Opondo.
Wenyeji walipambana kutafuta bao la kusawazisha, lakini Maniema ilifunga kila njia. Ilituma krosi, mipira ya kupenya na kona, lakini yote ilirudi bila mafanikio. Baadhi ya juhudi za mwisho za Nyambane na Lennox Ogutu hazikuzaa matunda.
Kipyenga cha mwisho kilithibitisha kipigo cha pili cha Nairobi United kwenye hatua ya makundi, ikiendelea kusalia mkiani bila pointi. Wydad na Maniema zipo juu na pointi sita kila moja, huku Wamorocco wakiongoza kwa tofauti ya mabao. Azam ya Tanzania, ambayo pia haijashinda, haina pointi kama Nairobi United.
Kichapo hicho cha Nairobi United, umeifanya timu ya DR Congo kuibuka na ushindi nchini Kenya kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1994, wakati DC Motema Pembe ilipoifunga Kenya Breweries 3-0 na kutwaa Kombe la Washindi Afrika. Imekuwa ni mara ya pili katika majaribio 10 kwa timu ya DR Congo kushinda ugenini dhidi ya timu za Kenya katika mashindano ya CAF. Pia imekuwa ni mara ya kwanza kwa Maniema kushinda mechi ya ugenini katika historia ya michuano ya CAF.