Kitaka haoo robo fainali Shishi Cup, Shika Adabu FC yatolewa

KITAKA FC ilifuzu robo fainali michuano ya Shishi Super Cup baada ya kuipepeta Vyemani United mabao 3-0 katika mechi iliyopigwa uwanja wa Panama iliyopo eneobunge la Likoni, kaunti ya Mombasa.

Alikua Sammy Omile aliyeleta furaha kwa mashabiki wa Kitaka FC akifungua ukurasa wa mabao dakika nne kisha Anafi Machafu na Hassan Kizianda wakapigilia misumari miwili zaidi  dakika ya 10 na 24 mtawalia.

Vyemani United ilizunduka kutoka usingizini kipindi cha pili na kuanza kulisakama lango la wapinzani wao lakini mashuti yao yalipanguliwa.

Veczula ambao haikuwa kwenye hesabu za mashabiki kutinga robo fainali, iliwashangaza wengi ilipoitandika Timbwani Villa mabao 3-1 kwenye mchezo wa hatua ya timu 16 bora.

Nao Vimbwanga, mojawapo ya timu kongwe zaidi katika eneobunge hilo, pia ilifuzu nane bora kwa kuisakama Zaragoza FC mabao 2-1 wakati Siren ikapiga hatua kwa kuilemea Shika Adabu FC 5-4 kupitia mikwaju ya penalti baada ya sare ya bao 1-1.

Timu nyingine iliyotinga robo fainali ni Panama FC baada ya kuwakomoa mahasimu wao Napoli FC kwa penalti 4-3 kufuatia mechi kumalizika sare tasa muda wa kawaida wakati Hope Rangers FC ikiidhalilisha Toronto mabao 2-1.

Bulls Wazee nao pia wamo robo fainali na leo Jumanne katika dimba la Shika Adabu itafahamika timu mwisho hatua ya nane bora kwa mechi inayokutanisha Scud FC dhidi  ya Chege Boys.