Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kilichosbabisha kifo cha beki wa Kakamega

KIFO Pict

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa tangazo rasmi la Kakamega Homeboyz, Abungana alifariki dunia alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali Kuu ya Kaunti ya Kakamega, siku chache baada ya kuichezea klabu yake katika mechi ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) dhidi ya Mara Sugar. Mechi hiyo ilipigwa Jumamosi iliyopita.

FAMILIA ya soka nchini Kenya imeingia katika maombolezo mazito kufuatia kifo cha beki wa klabu ya Kakamega Homeboyz, Silas Abungana.

Kwa mujibu wa tangazo rasmi la Kakamega Homeboyz, Abungana alifariki dunia alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali Kuu ya Kaunti ya Kakamega, siku chache baada ya kuichezea klabu yake katika mechi ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) dhidi ya Mara Sugar. Mechi hiyo ilipigwa Jumamosi iliyopita.

Taarifa zaidi zinadai, Abungana alifariki baada ya kushambuliwa na mdogo wake kufuatia mgogoro wa kifamilia, ambapo ndugu zake walidaiwa kumshinikiza amwache mkewe, ambaye hawakumkubali kama mkwe wa familia.

Kifo cha Abungana kimesababisha mshtuko mkubwa katika ngazi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF), huku klabu, wachezaji, maafisa na mashabiki wakionyesha huzuni kubwa kutokana na kumpoteza mchezaji aliyekuwa bado anacheza soka la daraja la juu.

KIF 01

Kakamega Homeboyz yathibitisha kifo hicho

Klabu ya Kakamega Homeboyz imethibitisha kuwa, Abungana alifariki dakika chache kabla ya saa 6 usiku wa jana Jumatano, Februari 4, 2026.

Klabu hiyo ilisema beki huyo alifariki kutokana na majeraha ya kichwa aliyoyapata wakati wa shambulio lililotokea usiku wa Jumanne, Februari 3  2026, ikiwa ni siku chache baada ya kucheza mechi ya Ligi dhidi ya Mara Sugar.

Kwa mujibu wa klabu, Abungana aliwahishwa katika Hospitali Kuu ya Kaunti ya Kakamega baada ya kushambuliwa na alikuwa akipokea matibabu, lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya.

Licha ya juhudi za madaktari, alifariki baadaye, jambo lililoiacha klabu na jamii ya soka katika huzuni kubwa.

“Klabu inathibitisha kuwa Silas alifariki dakika chache kabla ya saa sita usiku wa jana Jumatano, Februari 4, 2026 alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali Kuu ya Kaunti ya Kakamega, baada ya kufariki kutokana na majeraha ya kichwa aliyoyapata katika shambulio la usiku wa Jumanne, tarehe 3 Februari,” ilisoma sehemu ya taarifa ya klabu.

Homeboyz imeeleza kuwa kifo chake ni pigo kubwa na ikaomba heshima na faragha kwa familia wakati huu mgumu.

Klabu hiyo pia ilisema Abungana alikuwa mchezaji mwenye nidhamu, aliyejitolea na aliyeitumikia timu kwa fahari.

“Katika kipindi hiki kigumu sana, tunaomba kwa heshima faragha kwa familia ya Silas, wachezaji wenzake, marafiki na maafisa wa klabu tunapojaribu kukubaliana na msiba huu mkubwa. Klabu itatoa taarifa zaidi baadaye. Pumzika kwa amani, Silas,” ilihitimisha taarifa hiyo.

KIF 02

Historia ya Silas Abungana

Silas Shihemi Abungana alikuwa mchezaji wa kulipwa wa soka Kenya aliyekuwa akicheza nafasi ya beki.

Alianza safari ya soka la daraja la juu akiwa na Shabana FC, ambako alitumikia klabu hiyo kwa misimu kadhaa akiimarisha safu ya ulinzi.

Akiwa Shabana, alikuwa sehemu ya kikosi kilichopandisha timu hiyo hadi Ligi Kuu ya FKF msimu wa 2022-2023, mafanikio makubwa kwa klabu na hatua muhimu katika taaluma yake.

Katika msimu huo, Shabana ilitawala Ligi ya National Super League (Daraja la Pili), ikimaliza kileleni na kupata tiketi ya moja kwa moja kurejea Ligi Kuu ya FKF msimu wa 2023-2024.

Uhamisho wake ulionekana kama hatua ya maendeleo, ukimpa nafasi ya kuendelea kushindana katika kiwango cha juu cha soka la Kenya.

Akiwa Kakamega Homeboyz, alivaa jezi namba 31 na alicheza mechi kadhaa za Ligi kama sehemu ya safu ya ulinzi ya klabu.


KIF 03

Rambirambi kila kona, klabu zikimlilia

Klabu ya Mathare United ilitoa ujumbe wa rambirambi kufuatia kifo cha beki Silas Abungana.

Katika taarifa yao, waliielezea habari hiyo kuwa ya kusikitisha sana na wakatuma pole kwa familia ya Abungana, marafiki na wote wanaohusishwa na Kakamega Homeboyz.

“Hizi ni habari za kusikitisha sana. Mathare United inatoa pole kwa familia ya Silas, marafiki na wote wanaohusishwa na Kakamega Homeboyz FC. Mawazo yetu yako nanyi katika kipindi hiki kigumu. Pumzika kwa amani, Silas,” ilisema klabu hiyo.

AFC Leopards 'Ingwe' pia iliungana na familia ya soka Kenya kuomboleza kifo cha Abungana.

“AFC Leopards SC inaungana na jamii ya soka nchini Kenya kuomboleza kifo cha ghafla cha beki wa Kakamega Homeboyz FC, Silas Abungana. Pole za dhati kwa familia yake, marafiki na wachezaji wenzake. Pumzika kwa amani,” ilisoma taarifa hiyo ya Ingwe.