Kifo cha Raila Odinga, mechi saba Ligi Kuu ya Kenya za ahirishwa
Muktasari:
- Hatua hii imekuja kufuatia tangazo la Rais wa Kenya, William Ruto la kuwepo kipindi cha siku saba za maombolezo ya kitaifa na kuamuru bendera zote nchini humo zipeperushwe nusu mlingoti.
Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), limeahirisha mechi saba zilizokuwa zimepangwa kuchezwa wikiendi hii ikiwa ni kwa heshima ya Waziri Mkuu wa zamani, Raila Amolo Odinga, aliyefariki dunia leo Jumatano Oktoba 15, 2025 wakati akipatiwa matibabu nchini India.
Hatua hii imekuja kufuatia tangazo la Rais wa Kenya, William Ruto la kuwepo kipindi cha siku saba za maombolezo ya kitaifa na kuamuru bendera zote nchini humo zipeperushwe nusu mlingoti.
“Kufuatia tangazo la Serikali la siku saba za maombolezo ya kitaifa kwa heshima ya Waziri Mkuu wa zamani Mheshimiwa Raila Amolo Odinga, Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) linasitisha ratiba zote za ligi zilizopangwa katika kipindi hiki.
"Tunaungana na taifa zima kumuomboleza kiongozi huyu mashuhuri na mpenzi mkubwa wa soka la Kenya. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi,” imesomeka sehemu ya taarifa ya FKF iliyotumwa kwa vyombo vya habari.
Mechi saba za Ligi Kuu ya Kenya zilikuwa zimepangwa kuanza Jumamosi, Oktoba 18, 2025 ambapo Mara Sugar ilitarajiwa kuikaribisha Bidco United, huku APS Bomet ikiwa ugenini dhidi ya Kariobangi Sharks.
Jumapili, Oktoba 19, 2025, Kakamega Homeboyz ilipangiwa kuvaana na Ulinzi Stars, Tusker FC ingechuana na Murang’a Seal, KCB ilikuwa ikabiliane na AFC Leopards, huku Shabana ikitarajiwa kumenyana na Mathare United.
Jumatatu, Oktoba 20, 2025 ambayo ni Siku ya Mashujaa, Gor Mahia ilikuwa ipambane na Posta Rangers.