Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kenya Police yatinga CAF kuishtaki Al Hilal iondoshwe CAFCL

Muktasari:

  • Al Hilal imeitoa Kenya Police kwa jumla ya mabao 4-1 na kufuzu hatua ya makundi, ambapo droo inatarajiwa kufanyika Novemba 3, 2025 mjini Johannesburg, Afrika Kusini. Klabu hiyo ya Sudan ilishinda 1-0 katika mechi ya kwanza jijini Nairobi, Oktoba 17, 2025 kisha ikakamilisha kazi kwa ushindi wa 3-1 katika mechi ya marudiano iliyochezwa Benghazi, Libya, Oktoba 24, 2025.

Kenya Police FC, ina imani kwamba Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) litatoa uamuzi mzuri kwao baada ya kuwasilisha malalamiko dhidi ya Al Hilal Omdurman ya Sudan kwa madai ya kuwatumia wachezaji wasio halali katika mechi yao ya Raundi ya Pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu 2025–2026.

Al Hilal imeitoa Kenya Police kwa jumla ya mabao 4-1 na kufuzu hatua ya makundi, ambapo droo inatarajiwa kufanyika Novemba 3, 2025 mjini Johannesburg, Afrika Kusini. Klabu hiyo ya Sudan ilishinda 1-0 katika mechi ya kwanza jijini Nairobi, Oktoba 17, 2025 kisha ikakamilisha kazi kwa ushindi wa 3-1 katika mechi ya marudiano iliyochezwa Benghazi, Libya, Oktoba 24, 2025.

Kabla ya kuanza kwa mechi hiyo ya marudiano, Kenya Police iliwasilisha rasmi malalamiko ikipinga uhalali wa wachezaji watatu wa Al Hilal, mlinda mlango kutoka Burkina Faso, Soufian Farid Ouedraogo; beki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ernest Luzolo; na mshambuliaji wa Nigeria, Sunday Damilare Adetunji. Adetunji alifunga mabao mawili kwa Al Hilal katika ushindi wao wa pili.

Malalamiko ya Kenya Police yaliwasilishwa kwa nahodha wa Al Hilal ambaye aliyasaini kama ushahidi wa kupokea, kulingana na taratibu za CAF za kuwasilisha malalamiko.

Ndani ya saa 48 baada ya mechi, Kenya Police iliiandika CAF kuthibitisha kwamba imewasilisha malalamiko yao. Baadaye ilituma uthibitisho wa kina wa maelezo ya malalamiko hayo kulingana na mwongozo wa kanuni za CAF.

“Tumeshalipa ada ya malalamiko na tunatarajia suala hili litapatiwa uamuzi kabla ya droo ya hatua ya makundi,” amesema mwenyekiti wa Kenya Police FC, Nyale Munga, akizungumza na Nation Sport.

Ada ya malalamiko kwa CAF ni Dola za Marekani 2,000 (Sh5 milioni za Tanzania). Kenya Police watarejeshewa fedha hizo ikiwa malalamiko yao yatakubaliwa. Kinyume chake, CAF itatoza faini ya dola 10,000 (Sh24.9 milioni za Tanzania) kwa klabu hiyo.

Kenya Police inadai kuwa wachezaji hao watatu hawajasajiliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Sudan (SFA), hivyo hawakustahili kuchezea Al Hilal katika mashindano ya CAF.

“Kanuni zinasema wazi kwamba wachezaji wanaoshiriki mashindano ya CAF lazima wawe wamesajiliwa na shirikisho la taifa ambalo klabu yao imeunganishwa nalo,” amesema Munga.

Zaidi ya hapo, Kenya Police FC imedai kuwa Al Hilal ina wachezaji wageni 14 kwenye orodha yao, jambo linalokiuka kanuni za SFA zinazoziruhusu klabu kusajili wageni 10 pekee kwa kikosi cha kwanza. Klabu zinaweza kuongeza wachezaji watatu wa kigeni zaidi iwapo wana umri chini ya miaka 21 na wamesajiliwa kama wachezaji wa timu ya vijana.

Munga amesema walipata taarifa kuhusu wachezaji hao wasio halali kupitia msamaria mwema.

“Kuna watu katika soka la Afrika wanaotaka mambo yafanyike kwa usahihi, na mmoja wao alitupa taarifa kuhusu wachezaji wasio halali wa Al Hilal,” amesema Munga, akikataa kutaja vyanzo vyake, akiwaita tu watu wa Sudan wenye nia njema.

Iwapo malalamiko ya Kenya Police FC yatakubaliwa, CAF itabadili nafasi ya Al Hilal kwenye droo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu 2025–2026 itakayofanyika Jumatatu Novemba 3, 2025.

Kwa upande wao, Al Hilal imekanusha malalamiko ya Kenya Police ikisema hayana uzito wowote wa kweli, ikisisitiza wachezaji wao wamesajiliwa kihalali chini ya usimamizi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Sudan na CAF.

“Uongozi wa klabu umealikwa rasmi kushiriki kwenye hafla ya droo mjini Johannesburg. CAF pia imetutumia orodha ya viwanja vilivyoidhinishwa ili tuchague tutakakotumia kwa mechi zetu za nyumbani,” imesomeka taarifa ya Al Hilal.