Kagame Cup 2025 zawekwa Sh 814 Milioni
Muktasari:
- Michuano hiyo itakayoshirikisha klabu 11 za nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Michezo vya Afrika Mashariki na Kati (Cacefa) itafanyika jijini Dar es Salaam, huku Simba na Yanga zikichomoa kwa mara nyingine kutokana na kutingwa na ratiba ilizonazo kwa sasa.
ZAIDI ya Sh 800 Milioni zimewekwa katika michuano ya Kombe la Kagame 2025 inayotarajiwa kuanza kupigwa Septemba 2-15 kupitia mdhamini mpya aliyetangazwa asubuhi ya leo Alhamisi jijini Nairobi.
Michuano hiyo itakayoshirikisha klabu 11 za nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Michezo vya Afrika Mashariki na Kati (Cacefa) itafanyika jijini Dar es Salaam, huku Simba na Yanga zikichomoa kwa mara nyingine kutokana na kutingwa na ratiba ilizonazo kwa sasa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Cecafa iliyoachiwa hivi punde ni kwamba kampuni ya Betika ndio mdhamini mpya wa michuano hiyo ambapo yenyewe imeweka kiasi cha Sh 42 milioni za Kenya ambazo ni zaidi ya Sh 814 milioni za Kitanzania.
"Tunayofuraha kumtangaza mdhamini mpya wa michuano ya Kombe la Kagame kwa msimu huu wa 2025-2026," taarifa hiyo ya Cecafa inasomeka hivyo ikieleza hafla ya kusaini mktaba huo imefanyika leo asubuhi kwenye Ukumbi wa Pan Pacific Suites, iliyopio jijini Nairobi.
Makamu wa Rais wa CECAFA, Paulos Weldehaimanot alisema: "Ushirikiano huu unaonyesha nguvu ya mshikamano kati ya soka na sekta binafsi na unaonyesha imani ambayo chapa kubwa kama hii kuipa thamani na uwezo wa mashindano ya CECAFA,” alisema Weldehaimanot.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo iliyodhamini Kagame Cup, Mutua Mutawa alisema wamefurahi kusaini mkataba huo wa kuidhamini michuano hiyo na kwamba wameweka Sh 42 Milioni za Kenya, kwa lengo la kuunga juhudi za kuunga mkono maendeleo ya soka la ukanda huo wa Afrika Mashariki na Kari.
Msimu uliopita michuano hiyo iklidhaminiwa na Dar Port na Red Arrows ya Zambia ndio iliyobeba ubingwa kwa penalti 11-10 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1 dhidi ya APR ya Rwanda katika pambano kali la fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Kwa msimu huu, michuano hiyo inatarajiwa kuzishirikisha timu 11 baada ya Simba na Yanga kuchomoa tena kushiriki michuano hiyo kama ilivyokuwa msimu uliopita kutokana na kubanwa na ratiba walizonazo;
Timu zilizothibitisha baada ya Simba na Yanga kujiondoa ni; Vipers (Uganda), El Merriekh Bentiu (Sudan Kusini), Mlandege (Zanzibar), Al Hilal (Sudan), Kenya Police(Kenya), Ethiopia Insurance (Ethiopia), MCC FC (Somalia), APR (Rwanda), Aigle Noir (Burundi), Singida Black Stars (Tanzania) na ASAS Djibouti Telecom (Djibouti).