INGWE KULETA MTU TANO TU, KISA BAJETI

LICHA ya kupoteza  First 11 yake, uongozi wa klabu ya AFC Leopards unasema, utafanya usajili wa wachezaji watano  pekee.
Tayari imeshatambua wachezaji hao na kilichosalia ni kuondolewa kwa marufuku  waliyowekewa na FIFA  ya kutofanya usajili.
Dirisha la usajili litafungwa mwishoni mwa mwezi huu na kufikia wakati huo, Ingwe imepanga kuwa imesajili wachezaji watano wapya pekee.
Hii ni licha ya klabu kupoteza jumla ya wachezaji 17, waliogura kutokana na msoto  ulioikumba klabu.
Uongozi umeamua kusajili wachache hao, ikiwa ni mkakati wa kubana matumizi ili kuwapunguzia mzigo wa kifedha.
Kwa mujibu wa hesabu za Ingwe zilivyo, watano hao, wataongeza nguvu kikosi kipya cha msimu huu ambacho kinajumulisha wachezaji wa timu yao chipukizi waliopromotiwa hadi kikosi cha kwanza.
Kulingana na mwenyekiti Dan Shikanda, tayari klabu imeanza utaratibu wa kiwalipa wachezaji wao wa zamani pamoja na kocha Casa Mbungo fidia zao wanazowadai. Shikanda anasema wanachosubiria ni kuondolewa kikwazo hicho na FIFA baada ya kutimiza matakwa ya kulipa fidia hizo.
"Tunachosubiri kwa sasa ni kibali kutoka kwa FIFA ili tuweze kuwasajili wachezaji angalau watano ambao tayari tumeshawatambua."Shikanda anasema huku akidinda kutaja majina.
Kulingana na naibu kocha Tom Juma, Ingwe inapania kusajili viungo watatu, wingá mmoja na kipa mmoja.
"Kwa sasa siwezi kutoa majina ya wachezaji  hao wapya ila ninachojua ni wanakuja watano kuimarisha kila safu. Lakini pia hatusajili wengi ili tuweze kudhibiti bajeti yetu kama timu." Juma anasema.
Kulingana na mdokezi wetu, Ingwe tayari imeanza mazungumzo na wingá wa Gor Mahia Clifton Miheso pamoja na straika wao wa zamani John Mark Makwatta aliyeyoyomea Zambia. Pia inamwinda kiungo Duncan Otieno.
Miheso amegoma kurefusha mkataba wake na Gor naye Makwatta akiwa na hamu ya kurejea nyumbani baada ya kuchemsha Zambia. Makwatta aliikacha Ingwe na kuelekea zake Zambia lakini sasa yupo tayari kurudi kujaza nafasi aliyomwachia Elvis  Rupia alipondooka. Rupia naye alitimkia zake Uarabuni.
Ingwe pia haina mlinda lango mzoefu baada ya kipa wao mkongwe Benjamin Ochan kurejea kwao Uganda huku walinda lango wa akiba John Oyemba na Ezekiel Owade nao wakijitoa baada ya mikatabaya yao kuisha.