Inauma lakini itabidi wazoee...

ILIANZA na Posta Rangers kisha ikafuata FC Talanta, Kenya Police FC na AFC Leopards, sasa ni zamu ya Gor Mahia, Bidco United na Kariobangi Sharks kukaa pembeni wikendi hii mechi za Ligi Kuu Kenya zikiendelea.

Kinachofanya timu hizi zisishuke uwanjani kwenye ngarambe za FKFPL inatokana na kukabiliana na timu ambazo zinasubiri ‘huruma’ ya Mahakama ya Usuluhishi Migogoro Michezoni (SDT).

Mathare United na Vihiga Bullets zilishushwa daraja msimu uliyopita huku Wazito FC wakilazimika kucheza playoff kujinusuru panga la kushushwa lakini timu zote zikarudishwa kukipiga msimu huu wa FKFPL kufuatia Kamati ya Utendaji Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kufuta matokeo ya msimu uliyopita uliyosimamiwa na Kamati ya Mpito FKF.

Mabingwa wa Supa Ligi ya Taifa (NSL) msimu uliyopita, APS Bomet ambayo ilipanda daraja kucheza FKFPL lakini ikarudishwa NSL, iliwasilisha malalamiko yao mbele ya SDT kupinga matokeo ya msimu uliyopita kufutwa na sasa wanasubiri maamuzi ya SDT.

FKF imesisitiza msimu mpya wa FKFPL utaendelea kama ilivyopangwa kwenye ratiba lakini mechi zinazohusu timu zinasubiri maamuzi ya SDT ndizo zitakuwa zinahairishwa.

Mabingwa wa kihistoria, Gor Mahia ambao wameanza msimu vizuri wakishinda mechi zote mbili, yamepunguzwa momentum na hawatakuwa na mechi za ushindani kwa wiki mbili zijazo.

K’Ogalo walikuwa wamepangiwa kucheza na Wazito FC wikendi hii kisha wiki ijayo waikabili Mathare United, lakini sasa watasubiri hadi Desemba 17 kushuka uwanjani kuvaana na Kariobangi Sharks.

“Mechi zetu mbili za ligi zilizokuwa zipigwe Desemba 3 na Desemba 11 dhidi ya Wazito na Mathare United mtawalia zimehairishwa kusubiri kesi iliyopo mbeleni mwa SDT; tunarudi dimbani Desemba 17 dhidi ya Sharks,” ilisomeka taarifa ya K’Ogalo kwenye mtandao wao wa kijamii.

Mechi zingine za FKFPL zilizoota mbawa wikendi hii ni Bidco United dhidi ya Vihiga Bullets na Sharks waliyokuwa wacheze na Mathare United.