Huko mkiani watatoana roho

ENDAPO Vihiga Bullets wakishida mechi zao zote za Ligi Kuu Kenya, watamaliza msimu wakiwa na pointi 35 hivyo kumaanisha timu zote zilizopo chini ya Posta Rangers FC iliyo na pointi 35 zipo hatarini kushushwa daraja.

Hii ni hesabu ya vidole tu kuelekea mbio za kuepuka kushushwa daraja huku FKFPL ikiingia raundi ya 26 wikendi hii na zikiwa zimebaki mechi nane kuhitimisha msimu.

Hali sio shwari kwa Vihiga Bullets waliyorudishwa kwenye mikikimikiki ya FKFPL licha ya kushushwa daraja msimu uliopita kutokana na ligi hiyo kufutwa.

Tayari timu hiyo yenye maskani yake magharibi mwa Kenya inayoburuza mkia imesusia gemu mbili na kama itaingia mitini tena basi itakuwa rasmi imeshushwa daraja.

Kocha wa Vihiga Bullets, Milton Kidiga, anakiri ni vigumu kuepuka kushushwa daraja hususan baada ya timu yake kuchezea kichapo cha mabao 5-2 kutoka kwa Nairobi City Stars na jana tena walipoteza mabao 4-0 dhidi ya Police FC.

“Jukumu (kubaki FKFPL) linazidi kuwa gumu lakini tunahitaji kuwa na imani, kupambana, na kikubwa zaidi kuanza kushinda mechi mfululizo,” alinukuliwa kocha huo.

Naye kocha wa Wazito FC, Charles Odera, ambaye timu yake jana ilikua inacheza mchezo wao wa kiporo dhidi ya mabingwa watetezi Tusker FC, alisema watapabana hadi kieleweke.

“Hatukati tamaa kubaki FKFPL, na mtu yeyote asitarajie pointi za bwerere kutoka kwetu, mechi zilizobaki bado ni nyingi na hatuko tayari kunyoosha mikono,” alitahadharisha kocha Odera.

Timu nyingine hatarini kuangikiwa na shoka la kushushwa daraja ni Mathare United ambapo kama ligi itamalizika leo, basi watacheza playoff kuweka hai matumaini ya kubaki FKFPL.

Mathare United haikuwa na mwanzo mzuri wa ligi msimu huu na mambo yalionekana kubadilika uongozi ulipomkabidhi Samuel Koko mikoba ya kuinoa timu hiyo kutoka kwa Boniface Omondi.

Kocha huo kinda alibadili upepo akipata ushindi katika mechi sita ikiwemo dhidi ya vigogo Gor Mahia na AFC Leopards, lakini mwelekeo ukapotea katika mechi tatu za mwisho ambazo walifungwa na kushindwa kupata bao.

“Siwezi kudanganya na kusema hatuna presha, tunapigana kubaki kwenye ligi na tunafanya kadri tuwezavyo kurekebisha makosa yetu kwa gemu tunazocheza,” alisema Koko.