Hizi ndizo hesabu za Chipo Mtibwa Sugar
Muktasari:
- Mtibwa Sugar mara ya mwisho kupoteza mechi ilikuwa dhidi ya Yanga, ilipokubali kichapo cha mabao 2-0, Oktoba 28 mwaka jana, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
BAADA ya kuiongoza Mtibwa Sugar kukusanya pointi 15 katika mechi saba bila kupoteza, ikishinda mechi nne na sare tatu, kocha Yusuf Chipo amesema bado anapambana kuifanya iwe kati ya timu bora na shindani msimu huu kwa kuendeleza rekodi ya ushindi.
Mtibwa Sugar mara ya mwisho kupoteza mechi ilikuwa dhidi ya Yanga, ilipokubali kichapo cha mabao 2-0, Oktoba 28 mwaka jana, mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chipo amesema siyo rahisi kupata matokeo bora, bali ni mkakati mzuri wa benchi la ufundi na wachezaji kuhakikisha wanatengeneza mazingira mazuri ya kumaliza ndani ya nafasi tano za juu mwisho wa msimu.
“Ligi, kama inavyoonekana, ni ngumu; timu zimejipanga kwa kufanya sajili bora na za ushindani. Nafikiri ubora unaoonyeshwa na timu kwa sasa unatokana na kila mmoja kufanya majukumu yake kwa usahihi kuanzia uongozi, benchi la ufundi na wachezaji kwa ujumla wao,” amesema kocha huyo.
“Hakuna kinachoshindikana mbele ya mikakati imara. Naiona timu yangu ikiendeleza ubora kwa kuwaheshimu wapinzani tunaokutana nao. Soka ni mchezo wa nidhamu; ili kuwa bora au kudhibiti mbinu za mpinzani ni kuingia kwa kumheshimu na kuwa na mikakati imara ya ushindani, ndicho kitu tunachokifanya.”
Chipo amesema timu haitaki kufanya makosa kwa kurudia waliyoyafanya msimu walioshuka daraja, na wana mikakati imara ya kuwa bora na kuendelea na rekodi ya kutokuwa timu ya kugawa pointi kwa wapinzani.
Kocha huyo amesema licha ya kupata matokeo yanayowapa pointi muhimu, ana kazi kubwa ya kufanya kujenga safu imara ya ushambuliaji ambayo itatumia kila nafasi watakazotengeneza.
“Hatuna wastani mzuri wa kushinda mabao mengi kwenye mchezo mmoja. Pointi ni muhimu, lakini pia mabao mengi yanaongeza ushindani; tunaweza kukusanya pointi, lakini mabao yakawa kikwazo katika kinyang’anyiro cha nafasi tano za juu.”
Mechi saba za Mtibwa Sugar baada ya kipigo kutoka kwa Yanga ambazo wamepata matokeo mazuri ni suluhu dhidi ya KMC, ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya TRA United, sare ya suluhu dhidi ya JKT Tanzania, sare ya 1-1 dhidi ya Simba, ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City, ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Pamba Jiji na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons.