Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hesabu za Harambee Starlets ikiikabili Gambia kufuzu WAFCON

Muktasari:

  • Mchezo wa marudiano utafanyika Jumanne, Oktoba 28, 2025 katika Uwanja wa Lat Dior, uliopo Thiès, Senegal, ambako Gambia watakuwa wenyeji kutokana na viwanja vyao kukosa viwango vinavyohitajika na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Beki wa Harambee Starlets, Ruth Ingosi, ametoa wito kwa mashabiki kuunga mkono timu hiyo wanapojiandaa kwa mchezo muhimu wa mkondo wa kwanza wa kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 dhidi ya Gambia, utakaopigwa kesho Ijumaa Oktoba 24, 2025 saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Nyayo, Nairobi.

Mchezo wa marudiano utafanyika Jumanne, Oktoba 28, 2025 katika Uwanja wa Lat Dior, uliopo Thiès, Senegal, ambako Gambia watakuwa wenyeji kutokana na viwanja vyao kukosa viwango vinavyohitajika na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Mchezo huo ni wa kihistoria kwa Starlets kwani timu itakayoshinda kwa jumla ya mabao katika mikondo miwili itafuzu fainali za WAFCON zitakazofanyika Morocco kuanzia Machi 17 hadi Aprili 3, 2026.

Ingosi, ambaye kwa sasa anachezea Simba Queens ya Tanzania katika Ligi Kuu ya Wanawake, amesema: “Naomba mashabiki watuunge mkono kama wanavyounga mkono Harambee Stars. Tunatarajia kushinda mechi zote, nyumbani na ugenini.”

Mshambuliaji Violet Nanjala, anayekipiga United Eagles FC ya Saudi Arabia kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Municipal de Laayoune ya Morocco, naye ametoa ujumbe wa matumaini akisema: “Kwa msaada wa mashabiki tutashinda. Mungu yuko pamoja nasi. Timu imejiandaa vizuri.”

Kocha Beldine Odemba ameweka kambini kikosi cha wachezaji 40, ambacho kimekuwa kikijifua katika Uwanja wa Kasarani kwa takriban wiki tatu, na kufikia jana, wachezaji wote walikuwa wameungana kambini.

Ingosi, aliyewahi kuchezea Eldoret Falcons, Lakatamia FC (Cyprus) na Athlitiki Enosi Lemesou (Ugiriki), amesema: “Tumekuwa tukifanya mazoezi kwa zaidi ya wiki tatu, na ninaamini katika kazi tuliyofanya. Tumejiandaa na tumejipanga kushinda hapa nyumbani.”

Nanjala ana matumaini Kenya itarejea katika mashindano hayo kwa mara ya pili ndani ya muongo mmoja: “Tupo kwenye hatua za mwisho za maandalizi. Tuko tayari na tunawasubiri. Hii itakuwa nafasi nzuri kwa baadhi yetu kucheza AFCON kwa mara ya kwanza. Mechi ya Ijumaa haitakuwa rahisi, lakini tumeazimia.”

Jumapili iliyopita, kocha wa Gambia, Mariama Sowe alitangaza kikosi cha wachezaji 23 kwa ajili ya mchezo dhidi ya Kenya. Timu hiyo imekuwa ikifanya mazoezi katika Uwanja wa Serekunda East Mini, Gambia, tangu Agosti 2025.

Timu ya Gambia, inayojulikana kama Scorpions, inatafuta kufuzu kwa mara ya kwanza katika historia yao baada ya kushindwa kufanya hivyo katika miaka ya 2018, 2022 na 2024. Kikosi chao cha mwisho kinajumuisha wachezaji watano wanaocheza nje ya nchi:

Viungo Mariama Cham (AS Bambey FC, Senegal), Manyima Stevelmans (Riga FC, Latvia), na Fatoumata Kanteh Cham (Sevilla FC, Hispania). Beki Ola Buwaro (Lokomotive Moskva, Urusi) na Mshambuliaji Mam Drammeh (AS Bambey FC, Senegal).

Harambee Starlets walifika hatua hii baada ya kuiondoa Tunisia kwa jumla ya mabao 1-0 Februari 2025, wakitoka sare tasa 0-0 jijini Nairobi na kushinda 1-0 mjini Sousse, bao pekee likifungwa na Tereza Engesha.

Kwa upande wa Gambia, waliibwaga Niger kwa jumla ya mabao 4-1, wakishinda 2-0 ugenini Niamey na 2-1 walipokuwa wenyeji nchini Senegal.