Harambee Starlets yaichapa Gambia, yafuzu WAFCON 2026
Muktasari:
- Mechi hiyo ya marudiano ilipigwa Stade Lat Dior, Thies, nchini Senegal, kutokana na Gambia kukosa uwanja ulioidhinishwa na CAF kwa michezo ya kimataifa.
Timu ya Taifa ya Soka Wanawake ya Kenya, Harambee Starlets, imefuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (Wafcon) 2026, baada ya kuichapa Gambia bao 1-0, jana Jumanne Oktoba 28, 2025.
Mechi hiyo ya marudiano ilipigwa Stade Lat Dior, Thies, nchini Senegal, kutokana na Gambia kukosa uwanja ulioidhinishwa na CAF kwa michezo ya kimataifa.
Kenya imesonga mbele kwa jumla ya mabao 4-1, baada ya kushinda mechi ya kwanza 3-1 mjini Nairobi, Ijumaa iliyopita Oktoba 24, 2025 kwenye Uwanja wa Nyayo.
Kocha Benson Omondi Odemba, alifanya mabadiliko kadhaa kwenye kikosi chake kilichoanza dhidi ya Gambia jijini Nairobi, hasa katika safu ya ulinzi.
Vivian Nasaka aliingizwa kikosini kuchukua nafasi ya Elizabeth Muteshi, huku Tabitha Amoit naye akianza badala ya Lorine Ilavonga.
Lilian Awuor aliendelea kuwa golini, akitoa utulivu nyuma. Nahodha Ruth Ingosi na Enez Mango waliendelea kuwa nguzo muhimu katika safu ya ulinzi, wakiongoza kwa uzoefu na uimara.
Katikati ya uwanja kulikuwa na Mwanahalima Jereko, Ann Akinyi, na Martha Emedot, huku safu ya ushambuliaji ikijumuisha Elizabeth Wambui, Sheylene Opisa, na Fasilah Adhiambo waliokuwa na jukumu la kutafuta mabao.
Kwa upande wa Gambia, kocha Mariama Sowe alifanya mabadiliko saba kwenye kikosi chake. Kipa Mary Gomez, ambaye alikuwa benchi jijini Nairobi, alianza mechi hii akiwa langoni. Walinzi walikuwa Juana Colley, Bintou Ceesay, na Kaddy Jallow.
Safu ya kiungo iliundwa na Wuday Colley, Kouday Jallow, Kaddy Jattah, na Manyima Stevemans, huku washambuliaji wakiwa Teanteh Cham, Jallow Kaddy, Jammeh Fatoumata, na Jarju Sarah.
Kipindi cha kwanza kilikuwa na upinzani mkali, huku timu zote zikijaribu kupata bao. Gambia ndiyo ilikuwa hatari zaidi, ikilitia presha lango la Kenya mara kwa mara.
Hata hivyo, Awuor alionyesha umahiri wake kwa kuokoa hatari, akizuia mashambulizi ya Gambia.
Wachezaji wa Gambia walikosa nafasi kadhaa za wazi, hasa kupitia mipira ya adhabu na kona, lakini nahodha Ingosi aliendelea kuwa nguzo imara, akitoka juu kutema mipira yote hatari.
Dakika ya 16, nahodha wa Gambia, Foutamata Minteh, alikaribia kuifungia timu yake baada ya kupiga shuti kali kutoka mbali, lakini mpira ulipaa juu ya mwamba wa goli kwa inchi chache.
Kenya ilikaribia kupata bao dakika ya 27 wakati Opisa alipata nafasi nzuri, lakini shuti lake halikwenda sawasawa. Dakika ya 35, mpira wa adhabu wa Amunyolletes ulilazimisha beki wa Gambia kuokoa mpira huo uliokuwa ukielekea nyavuni.
Kipindi cha kwanza kilimalizika bila bao, huku Starlets wakionekana kukosa nguvu ya kushambulia mara kwa mara.
Kenya walihitaji kuongeza kasi ya mashambulizi katika kipindi cha pili na hatimaye juhudi zao zikazaa matunda.
Dakika ya 50, Elizabeth Wambui alipiga mpira mrefu kutoka katikati ya uwanja kuelekea eneo la hatari la Gambia. Mchezaji wa Gambia na kipa Gomez walishindwa kuelewana, na Adam akaitegea nafasi hiyo, akipiga mpira wavuni na kuiweka Kenya mbele 1-0.
Bao hilo lilitosha kuwapa Harambee Starlets ushindi na tiketi ya kufuzu kwa Wafcon 2026.
Hii itakuwa ni mara ya pili kwa Harambee Starlets kushiriki WAFCON baada ya mwaka 2016 ambapo iliishia hatua ya makundi.