Gor Mahia yawapigia magoti wachezaji

MWENYEKITI wa Gor Mahia, Ambrose Rachier amewalilia wachezaji wa klabu hiyo kuacha kasumba ya kuishtaki klabu FIFA kila wanapotibuana.

Kauli yake imetoka baada ya Gor kukubali kuwafidia wachezaji wake wa zamani iliyowachuja pasi na kufuata utaratibu wa mikataba yao Sh6 milioni.

Gor wamefungiwa na FIFA kufanya usajili hadi Januari 2013 baada yao kukiuka agizo la shirikisho hilo kuwafidia wachezaji wake wawili iliyowatimua bila ya kuzingatia utaratibu mwafaka.

Kati ya wachezaji hao walioiletea ngori Gor ni pamoja na wing’a Mtanzania Dickson Ambudo, beki Mganda Shafiq Batambuze, kiungo Mghana Steven Owusu, kipa kutoka Mali Adama Keita, fowadi Sando Yangayay na pia kocha wao wa zamani Steven Polack.

Kwa kuwavunjia mikataba yao na kisha kushtakiwa FIFA, Gor waliamrishishwa kuwafidia wote hao zaidi ya Sh12 milioni. Ingawaje Gor walifanikiwa kuwafidia baadhi yao kama kocha Polack, walishindwa kufanya hivyo kwa wote na kuwasababishia marufuku.

“Hayakuwa malengo yetu kutowafidia lakini janga la Covid-19 lilitukwamisha. Wala haikuwa malengo yetu ya kutowalipa wachezaji mishahara yao. Tatizo hilo lilikuwa nje ya uwezo wetu sababu hatukuwa na hela. Langu ni kuwasihi wachezaji, wasiwe wepesi wa kutushtaki kwa FIFA mishahara yao inapochelewa wakati mwingine mambo nje ya uwezo wetu hutokea,” Rachier kasihi.

Kufuatia kupata udhamini mpya kutoka SportPesa, uongozi wa Gor sasa unapania kumalizana na madeni yote ya wachezaji ili marufuku dhidi yao iweze kuondolewa.

Katibu Mkuu wa K’Ogalo Sammy Ocholla alisema dili la miaka mitatu kutoka SportPesa la Sh240 milioni litawawezesha kufuta madeni yao yote kwa wachezaji.