GOR MAHIA NI KUBAYA JOH, WACHEZAJI KUHEPA

MANZE  pale Gor ni kubaya joh! Sintofahamu ndani ya klabu inaendelea kuvuruga matokeo ya timu. Kwa mara nyingine tena Gor walishindwa kusajili ushindi juzi Jumatano dhidi ya wanyonge  wa ligi Nzoia Sugar.
Ikiwa ni mechi ya raundi ya 11, Gor walitarajia ushindi lakini waliishia kuambulia sare ya kufungana goli 1-1 na Nzoia wanapambana kuhakikisha wanaepuka shoka la kuteremshwa daraja mwishoni mwa msimu.
Hii ilikuwa ni mechi ya nne mfululizo kwa mabingwa hao watetezi kushindwa kusajili ushindi baada ya kuanza msimu kwa kishindo.
Taarifa tulizofanikiwa kuzinasa kutoka ndani ya klabu ni kwamba kuna sintofahamu kubwa inayoendelea Gor kwa sasa na ndio inayothiri matokeo ya timu uwanjani.
Sintofahamu hiyo imesababishwa na msoto wa  klabu ambayo imejikuta ikishindwa kuwalipa wachezaji mishahara yao. Tayari baadhi ya wachezaji tegemeo wanaripotiwa kuwa wanajiandaa kuvunja mikataba yao punde tu dirisha dogo la usajili wa Januari utakapofunguliwa.
Mastraika Jules Ulimwengu, Benson Omala na viungo Ernest Wendo  na Petere Oudu wote wakiwa wachezaji wa first 11, ndio kwa sasa wanavumishwa zaidi na taarifa za kuwa kwenye mchakato wa kujitoa Gor. Haikuwa sadfa kwamba wanne hawa walikosa kushiriki mechi hiyo ya Nzoia.
Aidha kwa mechi ya pili mfululizo kocha Mark Harrison hakuwepo uwanjani kuwaonhoza vijana wake kwani angali bado kwao Uingereza.
Baada ya kuzuka kwa uvumi uliodai kuwa hana nia ya kurejea Gor kutokana na yale mazingira magumu yaliyoko pale, Harrison ametoa kauli na kusema kwamba sababu iliyomfanya kuchelewa ni kwa sababu alipatikana na Corona hivyo atalazimika kukaa kwenye karantini kwa siku kadhaa.
Hali sawia na hii ilikuta Gor msimu uliopita walioishia kupoteza wachezaji kadhaa katikati ya msimu akiwemo kiuongo fundi Kenneth Muguna aliyejiunga na Azam FC ya  Tanzania.  Ngori hiyo iliwapelekea Gor kushindwa kutetea ubingwa wao. Kwa sasa wapo katika nafasi ya saba kwa alama sita nyuma ya vinara KCB.