Chebet ajiondoa mashindano ya Mbio za Nyika
Muktasari:
- Kenya itatumia mashindano hayo ya siku moja kuchagua timu itakayoiwakilisha nchi katika Mashindano ya Dunia ya Mbio za Nyika ya 2026, yatakayofanyika Tallahassee, Florida, Januari 10, 2026.
Mshindi wa medali ya dhahabu mara kadhaa katika mashindano ya dunia ya mbio za nyika, Beatrice Chebet, hatashiriki Mashindano ya Taifa ya Mbio za Nyika yatakayofanyika Jumamosi Oktoba 25, 2025 katika Uwanja wa Michezo wa Eldoret nchini Kenya.
Kenya itatumia mashindano hayo ya siku moja kuchagua timu itakayoiwakilisha nchi katika Mashindano ya Dunia ya Mbio za Nyika ya 2026, yatakayofanyika Tallahassee, Florida, Januari 10, 2026.
Kocha mkuu wa Timu ya Polisi wa Kenya (Kenya Police Service), Isaac Kirwa, amefichua kuwa bingwa huyo mara mbili wa dunia ameomba kupewa ruhusa ya kutoshiriki mashindano ya taifa kwa sababu hajawa tayari kushindana.
Hata hivyo, Kirwa ana matumaini kuwa Chebet, ambaye alishinda mbio za kilomita 10 za wanawake wakubwa katika mashindano ya dunia ya mbio za nyika mwaka 2023 (Belgrade) na 2024 (Bathurst, Australia), atapewa wild card ili kumpa nafasi ya kutetea taji lake kwa mara ya tatu mfululizo nchini Marekani.
Chebet alitwaa taji lake la kwanza la dunia katika mbio za nyika mwaka 2023 huko Bathurst, Australia, baada ya kumpita Letesenbet Gidey wa Ethiopia aliyedondoka katika mstari wa mwisho wa kumalizia mbio, na hivyo kumpatia Kenya ushindi. Alitetea taji hilo mwaka 2024 katika mashindano yaliyofanyika Belgrade, Serbia.
Katika mashindano hayo ya Bathurst, ambapo pia alipata wild card, Chebet aliwaongoza Lilian Kasait, Margaret Chelimo na Agnes Ng’etich kufanikisha ushindi wa Kenya wa nafasi ya kwanza hadi ya nne.
Chebet ndiye mwanamke wa kwanza katika historia kushikilia mataji ya Olimpiki na Dunia katika mbio za mita 5,000 na mita 10,000, sambamba na rekodi za dunia katika umbali huo.
Baada ya kushinda medali mbili za dhahabu (mita 10,000 na mita 5,000) kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024, Chebet alirudia mafanikio hayo hayo katika Mashindano ya Dunia mjini Tokyo, akishinda tena matukio yote mawili.
Julai 5, 2025, Chebet alivunja rekodi ya dunia ya mita 5,000 katika mashindano ya Prefontaine Classic Diamond League huko Eugene, Oregon, baada ya kukimbia kwa muda wa 13:58.06. Kenya ilitumia mashindano hayo kuchagua timu ya Mashindano ya Dunia ya 2025, na Chebet akawa mwanamke wa kwanza duniani kukimbia chini ya dakika 14 katika umbali huo.
Mwaka 2024, aliseta rekodi mpya ya dunia ya mita 10,000 kwa muda wa 28:54.14 katika mashindano hayo hayo ya Eugene, yaliyotumika kuchagua timu ya Olimpiki. Alikuwa mwanamke wa kwanza duniani kukimbia umbali huo chini ya dakika 29.
Kadri muda unavyosonga kuelekea Mashindano ya Dunia ya Mbio za Nyika ya 2026, kocha Kirwa ameonyesha imani kuwa Mashindano ya Taifa yatakuwa ya ushindani mkubwa, na Kenya itachagua timu imara kuwakilisha taifa huko Florida.
Miongoni mwa watakaoshiriki mashindano ya Eldoret ni Maureen Chebor, Gladys Kwamboka, Nelly Cheptoo, Miriam Chebet na mwanariadha mkongwe Mercy Cherono.
Mji wa Eldoret, unaofahamika kama Jiji la Mabingwa, unajiandaa kuandaa mashindano haya kwa mara ya nne, huku hamasa kubwa ikishuhudiwa miongoni mwa wanariadha chipukizi watakaopambana na wakongwe.
Makamu wa Rais wa Shirikisho la Riadha Kenya (Athletics Kenya) anayesimamia mashindano, Paul Mutwii, ameeleza kuwa mashindano haya yameletwa mbele kutokana na muda mfupi uliosalia kabla ya mashindano ya dunia mwezi Januari.
“Tunataka kuchagua timu mapema ili tuwe na muda wa kushughulikia vibali vya kusafiri kwenye ubalozi wa Marekani. Pia, kufanya mashindano haya mapema kutawapa wanariadha walioteuliwa muda wa kutosha kujiandaa,” amesema Mutwii.
Wanariadha kutoka kanda 19 za Shirikisho la Riadha Kenya (AK) na vikosi vya taasisi watashiriki katika mashindano hayo. Timu kutoka matawi ya AK (Nairobi, Pwani, Nyanza Kusini, Nyanza Kaskazini, Magharibi, Kaskazini Mashariki, Bonde la Ufa Kaskazini, Bonde la Ufa Kusini, Bonde la Ufa ya Kati, Kati na Kusini) zitashindana, sambamba na wanariadha kutoka vyuo vikuu, Huduma ya Polisi wa Kenya, Huduma za Magereza, Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF), Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS), Huduma ya Wanyamapori Kenya (KWS) na Huduma ya Misitu Kenya (KFS).