Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Baada ya ubingwa wa StanChart Nairobi, Chepkorir azitolea macho mbio za dunia 

RIADHA Pict

Muktasari:

  • Mashindano ya World Marathon Majors ni mfululizo wa mbio tano maarufu zaidi duniani zinazofanyika kila mwaka katika miji ya Tokyo, Boston, London, Sydney, Berlin, Chicago na New York. Mwisho wa kila msimu wa WMM, mwanariadha bora wa kiume na wa kike hupokea zawadi ya Dola za Marekani, 500,000 (Sh1.2 bilioni za Tanzania) kila mmoja.

Bingwa mpya wa mbio za wanawake za kilomita 42 katika Marathon ya Standard Chartered Nairobi, Hellen Chepkorir kutoka Kapsabet, anaamini mafanikio yake ya hivi karibuni yatafungua milango ya kushiriki katika mashindano makubwa ya World Marathon Majors (WMM).

Mashindano ya World Marathon Majors ni mfululizo wa mbio tano maarufu zaidi duniani zinazofanyika kila mwaka katika miji ya Tokyo, Boston, London, Sydney, Berlin, Chicago na New York. Mwisho wa kila msimu wa WMM, mwanariadha bora wa kiume na wa kike hupokea zawadi ya Dola za Marekani, 500,000 (Sh1.2 bilioni za Tanzania) kila mmoja.

Chepkorir anaamini kuwa sasa yuko tayari kujiunga na ligi hiyo kubwa baada ya kuibuka mshindi kwa mara ya kwanza katika toleo la 22 la mashindano ya Standard Chartered Nairobi yaliyofanyika jana Jumapili Oktoba 26, 2025.

Mashindano ya mwaka huu yalivutia idadi kubwa ya washiriki, 30,602, waliokimbia kupitia Barabara ya Southern Bypass kabla ya kumalizia Uhuru Gardens.

Chepkorir alionyesha uwezo na uimara mkubwa alipowaacha wapinzani wake katika alama ya kilomita 25, na kushinda kwa muda wa saa 2:27:17, ushindi wake wa kwanza katika marathon baada ya majaribio saba.

Hii ilitokea sambamba na ushindani mkali wa wanaume ambapo Bernard Chepkwony kutoka Iten alirejea kwa kishindo baada ya kutumikia adhabu ya miaka miwili ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli, na kushinda kwa muda wa 2:11:01 baada ya kuwaacha washindani wake kilomita saba kabla ya kumaliza. Chepkorir na Chepkwony wote walijinyakulia zawadi ya Sh2 milioni za Kenya (Sh38.3 milioni za Tanzania) kila mmoja.

Chepkorir, aliyemaliza nafasi ya pili katika Marathon ya Porto Alegro nchini Brazil mwezi Aprili 2025, na ya nne katika Marathon ya Jiji la Nairobi mwezi Julai 2025, aliwashinda Naomy Chepkorir kutoka Iten na Scholastica Jepkemboi wa Kapsabet waliomaliza wa pili na wa tatu kwa muda wa 2:27:37 na 2:29:18.

“Huu ni ushindi wangu wa kwanza tangu nilipopanda kiwango hadi marathon kamili mwaka 2016 kutoka kwenye mbio za uwanjani. Hii (zawadi ya fedha) ndiyo fedha nyingi zaidi kuwahi kupata,” amesema Chepkorir.

“Inaonyesha niko tayari kuingia kwenye mashindano ya World Marathon Majors mwaka ujao,” aliongeza Chepkorir ambaye ndoto yake siku moja ni kushiriki Marathon ya Boston.

“Ninajifua katika maeneo yenye milima huko Kapsabet, hivyo nadhani ningeweza kufanya vizuri katika njia yenye milima kama ya Boston. Natumai nitapata nafasi hiyo baada ya mafanikio haya,” amesema mwanariadha huyo anayefundishwa na Kocha Richard Mutai.

Chepkorir, anayevutiwa na Peres Jepchirchir, bingwa wa Olimpiki wa 2020 na bingwa wa dunia wa 2025 katika marathon huku pia akiwa na mataji matatu ya World Marathon Majors (New York 2021, Boston 2022 na London 2024), amesema ataamua jinsi ya kutumia zawadi yake hiyo ya fedha mara tu zitakapoingia benki.

“Sikuwa na mashindano yoyote nje ya nchi, hivyo nikaamua kushiriki mbio hizi muhimu. Nilijiandaa vizuri tangu Marathon ya Jiji la Nairobi,” amesema Chepkorir mwenye umri wa miaka 31, mama wa mtoto mmoja, ambaye amefurahia kumaliza msimu wake kwa mafanikio.

“Fedha hizi ni nzuri, natumai nitazitumia kwa busara.”

Kwa upande wa wanaume, Chepkwony, ambaye alimaliza adhabu yake mwezi Februari 2025, ameshinda mbele ya Alex Chepkwik Saekwo kutoka Iten aliyemaliza wa pili kwa muda wa 2:11:26, huku Ezekiel Kemboi Omullo, bingwa wa Marathon ya Standard Chartered Singapore 2022, akimaliza wa tatu kwa muda wa 2:11:40.

“Adhabu ya dawa imenifunza mambo mengi. Wanariadha tunapaswa kuwa waangalifu na dawa tunazotumia,” amesema Chepkwony, akieleza kuwa matibabu aliyopata kwa jeraha la mguu na mzio ndiyo yaliyomsababishia matatizo hayo. 

“Sikuwa mwangalifu, na ilinigharimu.”

Chepkwony mwenye umri wa miaka 39, ambaye alishindwa kumaliza mbio za kilomita 21 wakati wa Marathon ya Jiji la Nairobi Julai 6, 2025 baada ya kurejea kutoka kwenye adhabu, sasa anatarajia kutumia zawadi yake ya fedha kuboresha maisha ya familia yake huko Kericho.

Katika mbio za wanaume za kilomita 21, John Kithuku kutoka Machakos lakini anayejifua Iten, aliibuka mshindi kwa muda wa 1:02:34, akimshinda Nahashon Kipsang aliyemaliza wa pili kwa 1:03:30, huku Gilbert Korir akimaliza wa tatu kwa 1:03:33.

“Sasa nataka kupanda hadi marathon mwaka ujao,” amesema Kithuku, aliyeshinda Betika Half Marathon mjini Eldoret mwaka 2024 kabla ya kumaliza nafasi ya sita katika mashindano hayo Julai 2025.

Bingwa wa Afrika wa mita 1,500 mwaka 2018 na 2022, Vinny Chebet, alianza kwa kishindo kwenye mbio za masafa marefu alipomaliza wa pili katika mbio za wanawake za kilomita 21 kwa muda wa 1:15:20. Chebet, ambaye pia ni bingwa wa Kombe la Bara la mita 1,500 mwaka 2018, alishindwa na Fridah Rerimoi aliyeshinda kwa muda wa 1:14:22.