AUSSEMS: RUPIA, TUPIA MABAO BANA

Saturday May 29 2021
ausems pic
By Mwandishi Wetu

LICHA ya Elvis Rupia  kuwapaisha AFC Leopards hadi nafasi ya pili kwenye ligi, kocha Patrick Aussems bado hajaridhishwa na ufungaji wa straika huyo.
Kwenye mechi hiyo ya kiporo iliyosakatawa Alhamisi, Rupia alifuta swara ya kutofunga goli katika mechi zake nne za awali, kwa kupachika bao la ushindi dhidi ya Mathare United.
Bao hilo la pekee katika mchezo huo,  Rupia alilipachika kunako dakika ya nane ya mchezo kwa kuachia kombora nzito na mguu wake wa kushoto, uliomlemea kipa Job Ochieng.
Halikuwa jaribio lake la kwanza kumtesti kipa huyo lakini kwenye mashuti yake takriban mannne, kuelekea langoni ni moja tu ndilo lililozaa matunda.
Na ingawaje ushindi huo uliwatoa kutoka nafasi ya tatu hadi ya pili wakiwa na alama sawa na vinara KCB 36, kocha Mbelgiji Aussems anahisi kuwa Rupia ana uwezo mkubwa wa kutupia magoli mengi baada yake kumshuhudia akishindwa kutumia nafasi za kutosha alizopata dhidi ya Mathare.
"Kazi ya straika ni kufunga mabao. Nafurahia Elvis alipata goli sababu huwa anapata fursa nyingi tu za kufunga ila ninachohitaji kuona ni akitumia fursa zote anazopata vilivyo kwa kutupia mabao zaidi. Nahitaji kumaliza mchezo kwa magoli mengi sababu huwezi kujua kinachoweza kutokea baadaye kwenye mchezo." Aussems kasisitiza.
Unaweza kuelewa kwa nini kocha Aussems ana presha hiyo hasa kwa straika wake tegemeo Rupia.
"Wajua tukishinda 1-0 au 9-0  alama bado ni tatu, ila baada ya wiki mambo yanaweza kuwa tofauti kabisa. Tulipoteza nafasi kibao za kufunga magoli zaidi na kwa kweli tunahitaji kuwa makini mno kwenye umaliziaji. Hili ni jambo muhimu sana." Mbelgiji huyo kaongeza.
Ushindi huo wa 1-0 uliwasukuma hadi nafasi ya pili iliyokuwa ikishikiliwa na Tusker walio na alama 35 baada ya mechi 17. Sasa Ingwe wapo sawa na vinara KCB kila mmoja akiwa na pointi 36 baada ya mechi 17 kila mmoja. AFC wangeshika usukani wa ligi kuu kwa mara ya kwanza msimu huu, endapo wangewashinda Mathare kwa magoli manne mtungi au zaidi. KCB wamesalia kileleni kwa tofauti ya mabao wakiwa na 13, huku Ingwe sasa wakiwa na 11 baada ya mchuano wa Mathare.


Advertisement