Aussems ampa tabasamu Matano

MAKOCHA Patrick Aussems wa AFC Leopards na Robert ‘Simba’ Matano wa Tusker FC wamekua na bifu lakini kwenye dabi la Mashemeji mwishoni mwa wiki iliyopita, Aussems atakua amemkuna Matano.

Akiwa hana kitu cha kupoteza kwenye mechi hiyo, mbinu za Aussems zimenogesha mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Kenya huku pointi nne zikitenganisha timu inayoongoza, Tusker FC, dhidi ya timu iliyo nafasi ya tatu, Nzoia Sugar.

Gor Mahia waliingia kwenye dabi la Mashemeji wakiwa wameshushwa kutoka kileleni hadi nafasi ya pili lakini walishindwa kurudi kileleni baada ya kuchezea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Leopards kwenye gemu ambayo miongoni mwa mafans walikua Rais William Ruto na kiongozi wa upinzani Raila Odinga.

Mabao ya Victor Omune na Maxwell Otieno yalitosha kumpa tabasamu Matano aliyekuwa jukwani kufuatilia ngarambe hiyo ambapo sasa hivi Tusker FC wanajinafasi kileleni mwa msimamo wa FKFPL wakiwa na pointi 64 huku zikiwa zimebaki mechi nne msimu kutamatika.

Bao pekee la Austin Odhiambo, aliyewahi pia kuichezea Ingwe, halikutosha kwa K’Ogalo kuendeleza ubabe wake dhidi ya Ingwe ambayo hatimaye imefuta uteja uliyodumu kwa miaka saba.

Huenda mechi hiyo ingemalizika kwa sare ya mabao 2-2 lakini mkwaju wa penalti iliyopigwa na Benson Omalla anayefukuzia Kiatu cha Dhahabu ilitoka nje.

Aussems alisema kabla ya mechi hiyo na ile ya awali dhidi ya Nzoia Sugar, atabadili kikosi chake kwasababu mawazo yake ameyaelekeza kwenye Kombe la FKF hatua ya nusu fainali, ila cha kutia moyo kwa mafans wa Ingwe ni kuona timu yao ikishinda gemu zote mbili.

Wakati Aussems akimfurahisha Matano kwa matokeo hayo, safari ya FKFPL imefikia kikomo msimu huu kwa Vihiga Bullets wakiteremshwa daraja rasmi kufuatia kichapo cha bao 1-0 tena wakiwa nyumbani mikononi mwa FC Talanta.

Vihiga Bullets watacheza Supaligi ya Taifa msimu ujao na sasa swali kuntu ni nani ataungana naye kati ya Mathare United na Wazito FC?

Wazito FC walipata ushindi muhimu wa mabao 2-1 dhidi ya Posta Rangers na kuwaondoa katika nafasi ya 16 Mathare United waliyopoteza mchezo wao wa mwishoni mwa wiki kwa bao 1-0 dhidi ya Kenya Police FC.