Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Agnes Ng’etich: Nitaileta rekodi ya dunia nyumbani

Muktasari:

  • Ng’etich alikuwa anajaribu kuvunja rekodi hiyo kwa mara ya pili na akasema kwamba upepo mkali uliokuwa ukivuma mbele ulimzuia kufanikisha azma yake.

“Tulieni, rekodi ya dunia inakuja.” Huo ndio ulikuwa ujumbe wa mwanariadha anayeshikilia rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 10, Agnes Ng’etich, kwa Wakenya baada ya kukosa kuvunja rekodi ya dunia ya nusu marathon kwa sekunde 16 tu mjini Valencia, Hispania, Jumapili Oktoba 26, 2025.

Ng’etich alikuwa anajaribu kuvunja rekodi hiyo kwa mara ya pili na akasema kwamba upepo mkali uliokuwa ukivuma mbele ulimzuia kufanikisha azma yake.

“Ilikuwa karibu sana, lakini bado mbali kidogo. Hata hivyo, nawahakikishia kwamba rekodi hiyo itakuja nyumbani hivi karibuni,” amesema Ng’etich.

Atajaribu tena kuvunja rekodi hiyo katika Nusu Marathon ya Lisbon Machi 8, 2026.

Mwaka jana, Ng’etich mwenye umri wa miaka 24, alikaribia kuivunja rekodi ya dunia inayoshikiliwa na Letesenbet Gidey ya muda wa 1:02:52, aliposhinda Nusu Marathon ya Valencia kwa muda wa 1:03:04, akiwa ni mashindano yake ya kwanza katika umbali huo.

Alijaribu tena Jumapili kwenye njia ile ile lakini akaambulia patupu. Hata hivyo, alitetea taji lake kwa muda wa 1:03:08, muda wa tatu kwa kasi zaidi katika historia, akiwashinda Fotyen Tesfay wa Ethiopia (1:05:11). Wakenya wengine Veronica Loleo (1:05:46) na Gladys Chepkurui (1:06:58) walimaliza katika nafasi ya tatu na ya nne mtawalia.

“Mwaka jana, mvua iliharibu hali ya mbio, lakini mwaka huu upepo mkali katika nusu ya pili ya mbio ulipunguza kasi yangu,” amesema Ng’etich.

“Nitajitahidi tena Lisbon, ambayo pia ni njia ya kasi. Natumai hali ya hewa itakuwa bora zaidi.”

Mara ya mwisho njia ya Lisbon kutoa rekodi ya dunia ya nusu marathon ilikuwa mwaka 2001, wakati Susan Chepkemei alipoibuka mshindi kwa muda wa 1:05:44, na kuwa Mkenya wa kwanza kuvunja rekodi hiyo.

Chepkemei alimzidi Elena Mayer wa Afrika Kusini aliyekuwa amekimbia kwa 1:06:44, na kuwa mwanamke wa kwanza duniani kukimbia nusu marathon chini ya saa moja na dakika sita. Mayer alikuwa amevunja rekodi mara tatu kabla.

Ng’etich amesema ushindi huu unahitimisha msimu bora usio na majeraha, tofauti na mwaka uliopita alipopitwa na nafasi ya kushiriki Michezo ya Olimpiki ya Paris kutokana na maumivu ya misuli.

Amesema kupokea wildcard kushiriki Mashindano ya World Cross Country yatakayofanyika Januari 10, 2026 mjini Florida ilikuwa ni nusu ya bahati na heshima kubwa kwake.

“Hiyo ilikuwa habari njema zaidi niliyoipokea kabla ya mbio za Jumapili, na nawashukuru wateuzi kwa kuniamini, maana si kila mtu hupata nafasi kama hiyo,” amesema Ng’etich.

Ng’etich alipata medali ya shaba katika mashindano ya Dunia ya Mbio za Cross Country mwaka 2023 mjini Bathurst, Australia, na nafasi ya nne kwenye toleo la 2024 mjini Belgrade, Serbia.

“Ninajua rafiki yangu na bingwa mtetezi, Beatrice Chebet, naye amepewa wildcard, lakini nataka kumwambia kuwa nina nia ya kupata taji hilo pia,” amesema Ng’etich.

Katika Mashindano ya Dunia mjini Tokyo mwezi Septemba 2025, Ng’etich alimaliza nafasi ya 15 kwenye mita 5,000 na nafasi ya nne kwenye mita 10,000, huku Chebet akishinda zote mbili.

Akiwa amezingirwa na wanariadha wa kiume, Ng’etich alianza mbio za World Athletics Gold Label kwa kasi kubwa, akipita alama ya kilomita 5 kwa dakika 14:38, muda uliokuwa mbali zaidi ya rekodi ya dunia. Alivuka alama ya kilomita 10 kwa dakika 29:28.

Baadaye kasi ikapungua alipofika kilomita 15 kwa dakika 44:36, bado akiwa ndani ya muda wa kuvunja rekodi ya dunia (1:02:43), ingawa mwishoni alihitimisha kwa kasi ndogo.