Siasa zatishia kuikaushia Homeboyz ganji

KLABU ya Kakamega Homeboyz imekuwa moja kati ya klabu dhabiti kutoka mkoa wa Magharibi tangu ilipopanda daraja kukipiga Ligi Kuu Kenya.

Kwa misimu mitatu iliyopita, Homeboyz wamekuwa wakitoa ushindani wa kisawasawa na msimu uliopita, walikaribia kutwaa ubingwa baada ya kuongoza ligi kwa kipindi kirefu sana. Walimaliza msimu kwa kutoshana alama na mabingwa Tusker FC lakini kuzidiwa kwa tofauti ya magoli manne.

Mikakati yao ya kuendeleza ubora huo, sasa ipo kwenye hali ya msukosuko kisa siasa.

Hii ni baada ya Seneta wa Kakamega, Bonny Khalwale, kuanza presha ya kuitaka serikali ya kaunti ya Kakamega kuacha kuidhamini klabu hiyo. Badala yake Khalwale kapendekezea kaunti kuanzisha klabu mpya kwa kutumia fedha hizo wanazozipeleka Homeboyz.

“Kakamega Homeboyz ni mali ya watu wawili, Gavana wa zamani wa Kakamega, Wycliffe Oparanya na mmiliki Cleophas Shimanyula. Kuendelea kuifadhili klabu hii, ni kuendelea kuwafaidi wawili hao na hii haistahili,” alisema Khalalwe.

Homeboyz ilisaini mkataba wa miaka mitatu wa udhamini na kaunti ya Kakamega wakati Oparanya alipokuwa ofisini japo sasa ofisi hiyo ipo chini ya Gavana mpya, Fernandes Barasa.

“Namsisitizia Gavana Barasa afutulie mbali mkataba huo na badala yake aanze mchakato wa kuunda klabu mpya na ahakikishe inamilikiwa na watu wa Kakamega,” aliongeza.