Mwalala bado yupo area

Mwalala bado yupo area

BAADA ya aliyekuwa kocha wa Kakamega Homeboyz, Bernard Mwalala, kudai klabu hiyo bado haijamalizana naye licha ya kutangaza kumtimua, sasa amejibiwa.

Mapema mwezi uliopita, mwenyekiti na mumiliki wa Homeboyz, Cleophas Shimanyula, alitangaza kumtimua Mwalala na benchi lake nzima la ufundi kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Hii ni licha ya Mwalala kuiongoza Homeboyz kumaliza katika nafasi ya pili msimu uliopita wakilingana na pointi na mabingwa Tusker FC.

Kufuatia taarifa hizo, Mwalala alikanusha kuchujwa akidai kuwa hajapokea barua yeyote ya kutimuliwa wakati uongozi wa Homeboyz ukianza mchakato wa kusaka kocha mpya.

Sasa Mwalala kawaamikia tena Homeboyz akidai wanapaswa kumpa barua ya kumvunjia mkataba wake rasmi kama kweli wamemchuja badala ya kuendelea kumzungusha.

“Ni zaidi ya mwezi sasa tangu wadai kunichuja, taarifa nilizozipata kupitia vyombo vyenu vya habari. Hadi sasa hawajarasimisha zoezi hilo kwa kunipa barua rasmi. Wameishi kunizungusha kila nikiwauliza kunaendaje. Wanadai eti hawakunitimu ila walioniomba nikae pembeni wakati hatukuwahi jadiliana hilo. Sijui wanajaribu ujanja gani na mimi,” alihamaki Mwalala.

Kauli ya Mwalala ilipata jibu kutoka kwa meneja wa timu, Boniface Imbenzi, aliyesisitiza hakuna aliyemtimua Mwalala wala benchi nzima la ufundi.

“Maelezo ya mwenyekiti yalikuwa wazi kabisa. Aliombwa akae pembeni kidogo na ndio maana amekuwa akipokea mshahara wake hadi sasa. Ninachojua ni kuwa mkataba wake utamalizika mwisho wa mwezi huu kwa hiyo mwambieni asubiri na kama ukimalizika na akose kupokea mawasiliano, basi anaweza kukanyaga kubwa kubwa,” alisema Imbenzi.

MWANASPOTI imebaini Homeboyz imeamua kuendelea kulimpa Mwalala stahiki zake hadi mkataba wake utakapomalizika ili kuepuka uwezekano wa kushtakiwa FIFA.