Ingwe yaipiga FIFA magoti

UONGOZI wa klabu ya AFC Leopards unasema Janauri 2023 ni mbali sana kuendelea kusubiri kuondolewa kwa marufuku ya FIFA.

Ingwe inatumikia adhabu ya kutosajili kwa misimu miwili kutokana na kukutwa na makosa ya kuwavunjia wachezaji wao wa zamani mikataba pasi na kufuata utaratibu. Marufuku hiyo ilianza kutekelezwa baada ya Ingwe kushindwa kuwafidia kwa wakati.

Na huku sasa marufuku hiyo ikitarajiwa kuisha kwenye dirisha la usajili la Janauri, uongozi wa Ingwe unahisi huko ni mbali sana na kuipigia magoti FIFA kuwaondolea ili waanze mchakato wa kufanya usajili mapema.

“Tayari tumeshatumikia marufuku ya msimu mmoja na ya pili inapaswa kuisha Janauri. Ila sisi tunataka marufuku iondolewe kufikia katikati ya mwezi huu wa Disemba. Tunaharakisha kumalizana na madeni ya wachezaji ambao walitushtaki FIFA ambao bado hatujamalizana nao,” alisema Katibu Mkuu, Gilbert Andugu.

Andugu anasisitiza kuwa mapema ndio best kwani kuondolewa kwa marufuku hiyo sasa kutawapa muda wa kutosha kuanza kuweka mikakati ya kuwasaka wachezaji wa kusajili.

“Unajua utaratibu wa maamuzi ya FIFA huchukua muda. Tukisubiri hadi Janauri inaweza kuchukua muda FIFA kuandika barua rasmi na hii huenda ikatuvurugia mipango yetu ya usajili. Ndio sababu tunaomba marufuku hiyo iondolewe kabla ya Januari,” alisema.

Ingwe ilidaiwa zaidi ya Sh10 milioni ilipowavunjia mikataba wachezaji Vincent Habamahoro, Soter Kayumba, Bienvenue Shaka pamoja na kocha Andre Casa Mbungo.