Bandari kutesti mitambo, Kiungo atua KCB

Friday August 05 2022
Bandari PIC
By Abdulrahman Sheriff

MOMBASA. BANDARI FC itaanza kucheza mechi ya kwanza ya kujipima nguvu siku ya Jumamosi ambapo inatarajia kupambana na Simba Apparel FC kutoka Mariakani, Kaunti ya Kilifi katika uwanja wao wa nyumbani wa Mbaraki Sports Club.

Kocha wa Bandari FC, Anthony ‘Modo’ Kimani, alisema jana kuwa watacheza mchezo huo dhidi ya Apparel inayoshiriki katika Ligi ya Taifa Daraja la Pili Kanda ya Kaskazini.

“Tunaanza kujinoa kwa mechi dhidi ya Apparel ambayo tunaimani itakuwa ya kupendeza na kwa kuwa timu hiyo iko kwenye ligi ya taifa, tunaamini itatupata ushindani mzuri katika harakati zetu za kuinoa timu yetu,” alisema Kimani.

Timu ya Bandari FC ilitarajiwa kupambana na Gor Mahia katika mchezo wa kirafiki wikiendi iliyopita katika tafrija ya ufunguzi wa uwanja mpya wa Ronald Ngala lakini watayarishi wakaamua kuiweka timu ya Mombasa Combined.

Kimani aliambia MWANASPOTI baada ya mechi hiyo, wanatarajia kwenda Nairobi kucheza mechi kadhaa za kujipima nguvu dhidi ya timu ambazo watapanga watakapofika huko lakini alidokeza watacheza na timu kubwa za ligi kuu.

Kuhusu usajili, Kimani amesema wametosheka na wachezaji waliowasajili na hivyo hawana mipango ya kusajili wachezaji zaidi kwa kipindi kilichobakia cha usajili ambacho kinakamilika mwishoni mwa mwezi huu.

Advertisement

“Tumeshafunga kusajili wachezaji kwani hawa tuliowasajili na wale waliokuwako, wanatutosha na tunaamini watatekeleza wajibu wao na kufanya vizuri kwenye mechi zetu za ligi kuu pamoja na za mashindano mengine tutakayopangiwa kucheza,” alisema mkufunzi huyo.

Wakati huo huo, kiungo wa timu hiyo, Danson Chetambe Namasaka, aliyekamilisha mkataba wake wa miaka mitatu kuichezea timu hiyo ya Pwani alithibitisha jana kujiunga na KCB FC ya jijini Nairobi.

Akiongea na MWANASPOTI kwa njia ya simu baada ya mazoezi na timu hiyo jana asubuhi katika uwanja wa KCB Sports Club, Namasaka alithibitisha kumwanga wino wa mwaka mmoja unusu kukipiga KCB inayofundishwa na Zedekiah ‘Zico’ Otieno.

“Nimesajiliwa na KCB kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi sita na katika kipindi hiki nitaichezea timu yangu mpya kwa moyo wote. Nitajitahidi kuwaridhisha maofisa wa benchi la ufundi pamoja na viongozi wa klabu,” alisema.

Mwanasoka huyo anasema daima atadumisha nidhamu na kufuata maagizo ya kocha pamoja na maofisa wengine wa benchi la ufundi na viongozi wa klabu kwani anaamini mchezaji sio kucheza vizuri lakini ni kuonyesha nidhamu ya hali ya juu.

Kuhusu kutoongezwa mkataba na Bandari FC, Namasaka alisema hayo ndiyo maisha ya mchezaji kutoka klabu moja kwenda nyingine na hana kinyongo na Bandari FC.

Mwenzake Collins Agade ambaye hakuongezwa mkataba na Bandari FC alisema yeye yuko Kisumu akipumzika na kusubiri kumalizika kwa uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti 9 na baada ya hapo atajihusisha na mambo ya soka.

Advertisement