Zoran awabana mastaa wake, awapa mambo matatu

KOCHA wa Simba, Zoran Maki amewabana mastaa wa timu hiyo kwa kuwataka wafanye mambo matatu yatakayowabeba kwenye ushiriki wao wa michuano mbalimbali ikiwamo mechi ya leo ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.

Yanga na Simba zitaumana kwenye mchezo huo wa kuzindua msimu mpya wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, utakaopigwa kuanza saa 1:00 usiku na Kocha Zoran alisema amewabana wachezaji wake kwa kuwataka watilie vichwani mwao mambo matatu muhimu.

“Jambo la kwanza nataka kutoka kwao ni nidhamu, la pili ni nidhamu na hata la tatu ni nidhamu ya kila kitu na nitakuwa mkali katika kuyasimamia hayo matatu,” alisema Zoran.

Zoran baada ya kueleza kauli hilo aliifafanua na kusema nidhamu ya kwanza anataka kuona kwa wachezaji wake kuzingatia muda wa kula wanapokuwa kambini hataki kuona hata dakika moja akipotea.

Alisema kama walipangiana kunywa chai ni saa 2:00 asubuhi wachezaji wote wanatakiwa kuwa eneo la kupata chakula ikitokea kuna mmoja ameingia zaidi ya hapo bila ya kuwa na sababu maalumu au ruhusa, hatamuelewa.

“Hivyo hivyo hata kwenye chakula cha mchana au kile cha usiku lakini nimewaeleza wakiwa nyumbani kwao wanatakiwa kula vyakula vizuri na sahihi kwa wachezaji ili kukwepa uzito kuongezeka,” alisema Zoran na kuongeza;

“Nimewambia wachezaji wangu wanatakiwa kuzingatia muda wa kuingia kambini jambo ambalo tulikubaliana au kuwapa taarifa wakati wanaondoka, sitakubali kuona mchezaji anaingia muda zaidi ya huo au hayupo kambini bila taarifa rasmi,”

“Wachezaji wanatakiwa kukwepa vitu ambavyo si vya msingi anapokuwa uwanjani hata nje kwenye maisha yake ya kawaida kwani hilo ni moja ya nidhamu, wanapaswa kufanana wanapokuwa kwenye jezi ya Simba au maisha ya kawaida.

“Katika maisha ya mpira na haya ya kawaida ni ngumu kufikia malengo mliyojiwekea kama hakutakuwa na nidhamu, ndio maana nataka kulisimamia hilo ili kuona tunafanya vizuri msimu huu.”

Katika hatua nyingine Zoran alisema anafahamu wachezaji wengi wa Afrika hawapendi kufuatiliwa na kuwekewa misingi kama hiyo ila kwake anataka kuwaona wachezaji wa Simba wanaishi maisha kama ya wachezaji wa Ulaya.

“Tukiishi katika misingi hiyo ya nidhamu kwenye kila kitu hiyo itakuwa ni moja ya silaha zetu za kufanya vizuri katika mashindano yote kama malengo yetu yalivyo,” alisema Zoran.