Musonda aaga rasmi mashabiki Yanga

Muktasari:
- Musonda ameitumikia Yanga kwa misimu miwili na nusu akitwaa mataji matatu ya Ligi na Kombe la Shirikisho pamoja Ngao ya Jamii mara mbili.
SIKU chache baada ya Mwanaspoti kuripoti kuwa mshambuliani, Kennedy Musonda hatakuwa sehemu ya kikosi cha Yanga kwa msimu ujao wa 2025/26 mwenyewe ameibuka na kuwaaga mashabiki na wanachama wa timu hiyo.
Musonda ameitumikia Yanga kwa misimu miwili na nusu akitwaa mataji matatu ya Ligi na Kombe la Shirikisho pamoja Ngao ya Jamii mara mbili.
Kupitia mtandao wake wa kijamii, Instagram ameandika “Wananchi, sijui niseme nini? Mmekuwa bora kwangu, kwa familia yangu na kwa ndoto yangu. Asante kwa kucheka na mimi, kuota na mimi, kushinda na mimi, na pia kulia na mimi.”
Kisha akaongeza; “Mtu fulani alisema kila hadithi nzuri lazima ikome, milele ntashukuru naondoka naenda kujaribu maisha sehemu nyingine.”
Akiwa Yanga, Musonda ameifungia mabao 34 na kutoa asisti 13 na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Musonda akiwa na Yanga amepata nafasi ya kucheza na washambuliaji mbalimbali ambao walishaondoka ikiwa ni pamoja na Fiston Mayele, Jean Baleke ambao hawapo tena na kikosi hicho mbali na kina Clement Mzize na Prince Dube.
Kuthibitisha kwake kuwa hatakuwa sehemu ya kikosi cha Yanga msimu ujao, ni wazi kuwa amekuwa mchezaji wa kwanza kujiweka kando ikiwa timu hiyo bado haijaanza kutoa taarifa za 'Thank You' kwa wachezaji.