Zlatko katika deni la imani Yanga SC

Muktasari:
Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajia kuanza Jumapili ya Septemba 6.
Dar es Salaam. Wakati Ligi Kuu Bara ikitarajiwa kuanza Jumapili, makocha wanne wataingia katika presha ya kutafuta matokeo ili waendelee kubaki salama.
Mbelgiji Sven Vandebroeck wa Simba, mserbia Zlatko Krmpotic wa Yanga na watanzania Zubery Katwila (Mtibwa Sugar) na Amri Said wa Mbeya City wamebeba matarajio ya mashabiki wengi wa timu zao hadi sasa.
Kuna sababu tofauti zinanowaweka makocha hao katika presha ya matarajio ya mashabiki, ikiwemo matokeo yao ya msimu uliopita na ubora wa vikosi vyao msimu huu.
Kwa upande wa Sven, msimu uliopita alipata mafanikio, ikiwemo kuiwezesha Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la FA, akiwa ametwaa Ngao ya Jamii msimu huu.
Licha ya mafanikio hayo, inadaiwa kuwa Sven ana misimamo yake migumu inayosadikiwa kuwa mtihani kwa baadhi ya viongozi wa vinara hao.
Habari zinadai kuwa hata hivyo ni kama viongozi wamemuwekea mtego wa kuhakikisha Simba inafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, lakini endapo itatolewa mapema anaweza kuwa katika mlango wa kutokea.
Simba imesajili Joash Onyango (Kenya), Chris Mugalu (Congo), Lally Bwalya (Zambia), Benard Morrison (Ghana) na watanzania Ibrahim Ame (Coatal Union), David Kameta (Lipuli), Charles Ilanfia (KMC).
Kocha mwingine ambaye atakuwa katika presha ni Mrsebia Zlatko Krmpotic wa Yanga, ambaye amewahi kuzinoa TP Mazembe ya Congo na Zesco ya Zambia.
Kocha huyu amejiunga na Yanga hivi karibuni akichukua mikoba ya Luc Eymael aliyetimuliwa kutokana na kauli zake za kibaguzi alizozitoa kwa mashabiki wa klabu hiyo.
Zlatko, ambaye ana sifa ya kutodumu na timu nyingi zaidi ya mwaka alisema kwake kipaumbele ni nidhamu na kazi.
Hata hivyo, usajili uliofanywa na uongozi wa klabu hiyo unamuweka mtegoni Zlatko katika kuhakikisha klabu hiyo inapata matokeo, kwani wana misimu mitatu bila ubingwa sasa.
Yanga imewasajili Farid Mussa (CD Tenerife), Tonombe Mukoko (Congo), Tuisila Kisinda (Congo), Bakari Mwamnyeto (Coastal Union), Waziri Junior (Mbao), Kibwana Shomari (Mtibwa Sugar), Abdallah Shaibu ‘Ninja’ (LA Galaxy), Zawadi Mauya (Kagera Sugar), Yassin Mustapha (Polisi Tanzania), Michael Sarpong (Ghana) na Carlos Fernandes Guimares ‘Carlinho’ wa Angola.
Sio makocha hao wawili tu wa kigeni walio katika resha pia kuna wazawa ambao nao wanatakiwa kujichunga mmojawapo akiwemo Amri Said wa Mbeya City.
Amri anatakiwa kufanya kazi kubwa ya kurudisha ubora kikosi cha Mbeya City, ambayo imekuwa ikisua sua kwa misimu mitatu mfululizo na imenusurika kushuka.
Pia, Kocha wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila anaingia katika makocha watakaokuwa katika presha kubwa ya matokeo mazuri msimu ujao kutoka na kikosi chake kufanya vibaya msimu uliopita.
Mara nyingi Mtibwa Sugar imekuwa ama ikianaza vizuri ligi na baadae kucheza kawaida au ikianza vibaya na kumaliza vizuri.
Beki wa zamani wa Yanga, Bakari Malima alisema msimu ujao kocha atakayekuwa katika presha kubwa ni wa Yanga, Mtibwa na Mbeya City.
“Kocha wa Yanga, Zlatko ndiye atakuwa katika presha kubwa zaidi kwani Yanga ina timu nzuri, hivyo ili kuwafurahisha mashabiki lazima ashinde mechi nyingi.
“Pia upande wa Katwila na Amri nao watakuwa na presha ya kupata matokeo mazuri msimu ujao kwa sababu msimu uliopita walifanya vizbaya ingawa kitu ambacho nawausia hasa hawa makocha wazawa wasikubali kufa na tai shingoni kama timu zao zina matatizo waseme kwa viongozi wao yatatulwe la sivyo mizigo ya lawama itakuwa inawaangukia kila siku”,alisema Malima.
Mchambuzi, Ally Mayay alisema kocha wa Simba Sven anatakiwa kuwa na muendelezo mzuri tu kwani kikosi chake hakijavurugwa, lakini presha kubwa itakuwa kwa kocha wa Yanga katika kusaka ubingwa.
“Zlatko ndiyo ana presha kutokana na usajili uliofanywa na klabu na kitendo cha mashabiki kujitokeza kwa wingi kuwapokea wachezaji wao nayo inampa deni kubwa la kuhakikisha timu inafanya vizuri.
“Kwa Mtibwa, wanatakiwa kujitathimini kwa zaidi ya miaka 10 nafikiri msimu uliopita ndio ulikuwa msimu mbaya zaidi kwa timu hiyo, kwani walisubiri hadi mechi ya mwisho kubaki kwenye ligi, hivyo Katwila anatakiwa kufanya kazi ya ziada kurejesha ubora wa timu yake,” alisema Mayay.