Nahodha Mashujaa azitaka pointi sita

Muktasari:
- Mashujaa ipo nafasi ya nane katika msimamo baada ya kucheza mechi 28 na kukusanya pointi 33 na imebakiza mechi mbili kumaliza msimu dhidi ya KMC itakayopigwa Juni 18 kisha kumalizana na JKT Tanzania Juni 22, zote kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma.
NAHODHA wa Mashujaa, Baraka Mtuwi amesema licha ya kutokuwa na msimu bora wachezaji wa timu hiyo wamepambana hadi kuifikisha hapo ilipo na wana kibarua kigumu kupambania pointi sita katika mechi mbili zilizobaki.
Mashujaa ipo nafasi ya nane katika msimamo baada ya kucheza mechi 28 na kukusanya pointi 33 na imebakiza mechi mbili kumaliza msimu dhidi ya KMC itakayopigwa Juni 18 kisha kumalizana na JKT Tanzania Juni 22, zote kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mtuwi alisema walikuwa na msimu mzuri mwanzo hasa mzunguko wa kwanza, lakini mara baada ya kuanza msimu wa pili mambo hayakuwa mazuri upande wao ila kutokana na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja wamepambana na wanaendelea kufanya hivyo ili kuiweka timu hiyo kwenye mazingira mazuri ya kucheza ligi msimu ujao.
“Huu ni msimu dume, ni mgumu sana hadi sasa uhakika wa bingwa nani zikiwa zimebaki mechi mbili, hakuna timu kushuka daraja pia imethibitika kwa timu mbili kutokana na pointi walizokusanya ukiangalia hadi sasa kuanzia nafasi ya sita kila atakayedondosha pointi anaweza kucheza playoffs,” alisema Mtuwi na kuongeza;
“Bado kuna vita ya kupambania pointi ligi itakaporudi hivyo kila timu inajiandaa kuonyesha ushindani. Kwa upande wetu kama wachezaji tunapambana kuhakikisha hatudondoshi pointi zote sita ukizingatia tuna faida kubwa ya kucheza kwenye uwanja wetu wa nyumbani.”
Mtuwi alisema hawana kazi rahisi kwnye hilo kilichopo ni kuhakikisha wanafanyia kazi maelekezo ya mwalimu ili waweze kuendana na kasi na kujiweka tayari kwa msimu ujao.