Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zinapoteza ladha taratibu

Makao makuu ya klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

Simba na Yanga zimeitangaza Tanzania nje ya mipaka yake. Ni busara kukaa kimya kwa dakika moja kuwakumbuka na kutoa heshima kwa waanzilishi na wapambanaji wa klabu hizi mbili waliotangulia mbele za haki ikiwa na kuienzi michango yao mizuri na iliyotukuka.

HAKUNA shaka Simba na Yanga ni miongoni mwa klabu kongwe za soka nchini. Ilitanguliwa kuzaliwa Yanga mwaka 1935 na mwaka uliofuata walifuata watani zao wa Msimbazi, kwa maana hiyo mwaka huu wa 2016 klabu hizo mbili zinasherehekea miaka kati ya 80-81. Kwa hakika klabu hizo zinastahili pongezi na heshima kubwa kwa kuwepo katika soka la Tanzania kwa muda mrefu tangu enzi za ukoloni mpaka Tanganyika ilipopata uhuru na leo tukiwa Tanzania.

Simba na Yanga zimeitangaza Tanzania nje ya mipaka yake. Ni busara kukaa kimya kwa dakika moja kuwakumbuka na kutoa heshima kwa waanzilishi na wapambanaji wa klabu hizi mbili waliotangulia mbele za haki ikiwa na kuienzi michango yao mizuri na iliyotukuka.

Busara zao ndizo zilizolifikisha soka letu kuwa msingi wa burudani, starehe, kazi na ajira kwa vijana wenye vipaji vya soka kutoka ndani na nje ya nchi yetu ambao sasa wanalipwa mishahara minono na inayowawezesha kuwa na maisha bora zaidi. Huku sisi wapenzi na mashabiki wa soka hususan wanazi na mashabiki tukifaidi burudani isiyo na kifani.

Ni vema tukajikumbusha sehemu tu ya historia ya klabu hizi mbili huku tukijaribu kulinganisha nyakati tofauti zilizokuwa nzuri na hata mbaya katika safari zao za kutafuta ubora, umaarufu, maendeleo ya soka ya timu zao, kiufundi na kiuongozi katika zama zile na sasa.

Hata hivyo, isingekuwa sahihi kuzungumzia muundo na mfumo wa uendeshaji wa sasa wa timu hizi mbili bila kulinganisha kipindi cha nyuma.

Tunapoziangalia timu hizi siku za nyuma kabisa miaka 1960 hadi 1970 kabla na baada ya timu hizi kugawanyika na kusababisha kuzaliwa kwa timu za Pan Africa na Nyota Nyekundu tunaona dhahiri juhudi na ufanisi mkubwa toka kwa viongozi shupavu wa kipindi kile. Viongozi wazalendo wa kweli wa klabu hizo kwa upande wa Yanga kulikuwa na kina Mangara Tabu Mangara, Mshindo Mkeyenge, Kiluvia, Shirazi Sharifu, Alhaji Juma Shamte, Paul Sozigwa, Sammy Mdee na wengine.

Kwa upande wa Sunderland (sasa Simba) nawakumbuka kina Musa Alibabu, Mikidadi Kasanda, Ismail Kaminambeho na wengineo wengi, kwa hekima na busara zao wakichagizwa na mapenzi ya dhati kwa klabu zao waliweza kufanikiwa kwa kushirikiana na wadau wengine muhimu akiwemo Mzee Abeid Amani Karume Rais wa Kwanza wa Zanzibar, walifanikiwa kujenga majengo ya klabu hizo yaliyosimama hadi leo katika mitaa ya Msimbazi kwa Simba na Twiga na Jangwani kwa Yanga.

Majengo hayo yakijengwa ni viongozi wachache sana wa sasa wa timu hizi waliopo madarakani walikuwa tayari wamezaliwa.

Ni dhahiri kwamba viongozi wa sasa hawaonyeshi kujifunza chochote kutoka katika historia za klabu hiyo. Leo hii majengo yaliyojengwa na viongazi wa zamani ambao hata elimu yao haikuwa kubwa sana kivile na wengi hawakuwa na utajiri au ukwasi mkubwa kulinganisha na viongozi wa sasa ambao wameshindwa kuendeleza. Yaani hata kuyapaka rangi majengo hayo imekuwa mbinde kweli baada ya miaka takribani 40 hadi 50 toka yakamilike.

Kwa mtu yeyote anayeamini katika maendeleo na kwa kuzingatia kuwa Yanga na Simba ni taasisi kubwa zenye mali zisizohamishika pamoja na mtaji mkubwa wa wanachama na wapenzi unowafanya wakopesheke, leo hii tungeshuhudia majengo yakiboreshwa au kubomolewa na kujengwa majengo makubwa ya kisasa na ya kibiashara (business complex).

Majengo ambayo yangezipaisha klabu hizo kutoka kwenye utegemezi na kuwa miongoni mwa klabu tajiri sana barani Afrika.

Viongozi vijana na matajiri wa zama hizi wameshindwa kujenga juu ya msingi uliowekwa na waasisi wa klabu hizi.

Nilishuhudia Yanga miaka ya 1970 katika kuendeleza makao makuu yao makuu ya klabu kila timu ilipofanya mazoezi, wanachama na wapenzi walikuwa wakichangishwa kiasi cha pesa kwa ajili ya mradi wa kujenga majukwaa ya uwanja wa Kaunda. Napenda kuamini pamoja na mafuriko yanayotokea kila mara katika eneo hilo Yanga, leo ingekuwa imefanikisha mradi huo zamani.

Mazoezi ya Yanga zama zile yalikuwa kivutio tosha kushuhudia wachezaji bora wazalendo miongoni mwa walio bora zaidi kupata kutokea katika historia ya soka la nchi hii wakifanya mazoezi chini ya kocha, Profesa Victorr Stanslescu kutoka Romania.

Kulikuwa na kina Maulid Dilunga, Sunday Manara, Abdurahman Juma, Gibson Sembuli, Jellah Mtagwa, Omari Kapera ‘Mwamba’ (Franco Nero), Elias Michael, Muhidin Fadhil, Leonard Chitete, Boi Wickens, Hassan Gobos, Bona Max na wengineo.

Wakali hao walisindikizwa na kikosi cha watoto cha kina Mohamed Rishad ‘Adolph’, Mohamed Ugando, Mohamed Mkweche, Gordian Mapango, Jaffar Abdurahman, Mohamed Yahya ‘Tostao’, Rashid Iddi ‘Chama’, Sidi Sululu na Juma Pondamali na wengine.

Hivi sasa baada ya miaka 45 hakuna hata mfano wa uwanja bora wa soka wala jukwaa Kaunda, kilichobaki ni madimbwi ya maji yaliyotuwama yanayohifadhi vyura, majoka na uchafu wa kila aina huku viongozi wa sasa wakiahidi kujenga uwanja wa mabilioni ya pesa katika eneo hilo ambalo leo hii linaonyesha kuwa na utata mkubwa wa kimazingira.

Viongozi hao hao wamekuwa wakipoteza muda mwingi kuparurana na kutumia mamilioni ya pesa wakigombea wachezaji kutoka nje ya nchi na wasiokuwa na maadili kama kina Emmanuel Okwi ambao wamezifanya klabu hizi chuma ulete kwa kujipigia hela kiulaini.

Kipindi kilichopita Simba na Yanga zilisimamia na kujikuta katika kujenga mambo haya ya msingi kama; Kujenga program madhubuti na imara ya vijana, Kutokutegemea wachezaji wa kulipwa kwa kuzalisha vijana na Kujenga vikosi imara cha wachezaji wa ndani walio na mapenzi kwa klabu na viongozi wazalendo.

Pia, ilijikuta katika kuanzisha programi zenye malengo ya kutawala soka la Afrika, viongozi wabunifu, wanachama na wapenzi waliojaa uzalendo, kujenga tabia ya ushindi unaojenga soka, heshima na ustaarabu, kuyachukua mazuri yote toka nje na ndani ili kujenga klabu imara na bora

Kualika timu za nje ya Bara la Afrika kama vile; Uingereza, Romania, Brazili, Urusi ili kuzipa timu zao uzoefu wa kimataifa.

Pia, zilikuwa zikitoa maandalizi bora kwa timu kabla ya ligi na yenye tija kwa kuzipeleka timu zao Ulaya na Marekani ya Kusini.

Hali ilivyo na upungufu ya sasa

Programu ya vijana zinapuuzwa na kama zipo ni za kubabaisha, Hakuna uwajibikaji na udhibiti katika uendeshaji wa timu toka kwa viongozi. Jukwaa la klabu kutumiwa vibaya na wasemaji upande wa Simba na Yanga, mbaya zaidi pale kila mtu anakuwa msemaji.

Kutegemea sana wachezaji na makocha kutoka nje na kuwapuuza wazawa. Timu kutokuzingatia kuwepo na wanasaikolojia (counselors) kuwajenga wachezaji wa ndani ili kuisaidia Tanzania kupata wachezaji bora wa timu ya taifa .

Yote haya yana uhusiano moja kwa moja na ukuaji wa soka nchini hususan uimarishaji wa mipango ya TFF ya muda mfupi, kati na mrefu unaolenga mchezaji mmoja mmoja ili kujenga timu za taifa imara.

Juhudi zote zinazofanywa na wadau hususan TFF hazitaweza kufanikiwa iwapo hakutokuwa na dhati ya makusudi kwa klabu hizi kubwa ambazo ndizo haswa zilizo na miundombinu sahihi.

Pale zitakaposhindwa kutimiza wajibu wao katika azma nzima ya kupandisha soka la nchi hii.

Historia inathibitisha kuwa klabu hizi zimewahi kuyafikia mafanikio makubwa sana kipindi cha nyuma miaka 1960 mwishonii 1970 hadi miaka 1990 mwanzoni bila hata ya kuwa na mchezaji mmoja wa kulipwa.

Kinyume na imani iliyojengeka sasa kuwa haiwezekani kupata mafanikio bila kuwepo wachezaji wa kulipwa (professional players) ndani ya timu.

Zama hizo ni Tanzania ndio iliongoza katika Afrika Mashariki kwa kutoa wachezaji wa kulipwa katika nchi za Ulaya kama Sunday Manara miaka ya 1979-1981 alicheza pale Uholanzi katika timu ya Heracles, Mohamed Tostao, Kassim Manara, Adolph Rishad, hawa walicheza Ligi Kuu katika nchi ya Austria wakifuatiwa na Nicodemus Njohole.

Kizazi cha dhahabu cha Simba wakati huo cha kina Khalid Abeid, Shaaban Baraza, Yussuf Kaungu, Idd Kibonye na baadaye Aluu Ally, Yanga Bwanga, Mohamed Salim wote walisajiliwa huko Abu Dhabi, UAE, huku Mwinda Ramadhani akielekea kule Cyprus.

Renatus Njohole hapa mwishoni alimalizia soka lake pale Uswizi (Switzland)

Hii ni kuthibitisha kuwa soka la nchi hii kwa mfumo wa zamani lilifanikiwa sana kuliko sasa.

Hivi sasa Tanzania imegeuzwa pipa la taka (garbage bin) kwa kupokea wachezaji wa kulipwa wasiokuwa na viwango na kwa mshangao hata wale wanaocheza ndondo au soka la mchangani.

Wachezaji kutoka Brazili walijaribu kuvamia nchini mwetu kutafuta ajira.

Wadau wa soka wangependa kuona mabadiliko chanya katika uendeshaji wa soka na siyo mbwembwe za magazetini na mbaya zaidi kutaka kuzitumia klabu hizi na mchezo wa mpira kuimarisha agenda zenu za kisasa siku zijazo. Soka ndio chakula chetu, usingizi wetu, starehe yetu na ndio maisha yetu.