ZFF yang’atwa sikio idadi waamuzi
SHIRIKISHO la Soka Zanzibar (ZFF) limeshauriwa kufanya mafunzo ya mara kwa mara kwa waamuzi ili kupata wale watakaoendana na idadi ya mechi zinazochezwa.
Ushauri huo umetolewa na Katibu Msaidizi wa timu ya Chuoni FC, Suleiman Shaaban Suleiman aliyesema uchache wa waamuzi unasababisha baadhi yao kuharibu michezo, hivyo ni vyema kuliangalia suala hilo kwa umakini mkubwa.
Alisema sio vyema kuona waamuzi wanaendelea kutofanya vizuri katika mashindano kwani husababisha kushindwa kumudu mechi, hivyo kuchoka na kuamua kuchezesha vibaya au kutokana na uchovu wanashindwa kumudu kutofasiri sheria za mchezo husika.
“Kawaida ya mpira waamuzi wanatakiwa kuwa wengi kuliko idadi ya mechi, Fifa (Shirikisho la Soka Duniani) wana waamuzi wengi mpaka wengine wanakaa mwaka mzima hawapati mechi hata moja,” alisema Suleiman.
Katibu huyo alisema kuwa na waamuzi wengi kutasaidia kuongezeka kwa umakini na pia ZFF itakuwa na nguvu ya kuwaondoa kwenye mashindano ikiwa wataharibu.
“Tuna waamuzi wachache, utakuta mwamuzi huyo kachezesha mechi jana na leo anachezesha au kachezesha saa nane na saa 10 tena, hili linachangia uwezo kushuka.”